Ahmed Khalfan Ghailani, raia wa Tanzania amefutiliwa mbali mashtaka yote ya njama na mashtaka yote ya mauwaji ya kila moja kati ya watu 224 walouliwa wakati wa mashambulio ya mabomu huko Kenya na Tanzania.
Jopo la mahakimu katika mahakama ya serikali kuu huko New York limempata na hatia ya kupanga njama ya kuharibu mali ya taifa la Marekani.
Ghailani alikua mshukiwa wa kwanza kutoka geraza la kijeshi la Guantanamo Bay, kufikishwa mbele ya mahakama ya kiraia kwa mashtaka 285 ya ugaidi kwa kuhusika na mashambulio ya mabomu ya ubalozi wa Marekani huko Nairobi na Dar Ea Salaam mwaka 1998.
Hivi sasa anakabiliwa na kifungo cha miaka 20 jela, na mawakili wake wanasema watakata rufa dhidi ya hukumu hiyo.
Katika taarifa iliyoandikwa waendesha mashtaka walisema, "Tuna heshimu uwamuzi wa mahakimu, na tunaridhika kwamba hivi sasa Ahmed Ghailani anakabiliwa na kifungo kisicho kua chini ya miaka 20 jela na uwezekano wa kupatiwa kifungo cha maisha kwa jukumu lake katika mashambulio ya ubalozi."
Mashahidi wa upande wa waendesha mashitaka walitoa ushahidi kwamba Ghailani alinunua lori lililotumiwa kwa ajili ya kushambulia ubalozi wa Dar es Salaam. Wapelelezi wa FBI waliambia mahakama waligundua mabaki ya miripuko iliyotumiwa katika duka alikofanya kazi mshtakiwa huko Mombasa.
Watetezi hawakusuta tuhuma kama hizo, lakini walimueleza Ghailani kua mtu aliyetumiwa na wale walofanya kitendo cha kushambulia.
Wakili wake Peter Quijano amesema, "Serikali ilibidi kuonesha kwamba alijua nini lengo la wapanga njama au uhalifu ambao anatuhumiwa na lini na wapi alihusika katika baadhi ya mambo yaliyotokea."
Kesi ya serikali ilikumbwa na pigo kubwa kata kabla ya kuanza pale hakimu Lewis Kaplan kukata usahidi kutoka Hussein Abebe, shahidi mkuu wa serikali, ambae alitarajiwa kutoa ushahidi kwamba alimuzia Ghailani miripuko iliyotumiwa katika mashambulio ya mabomu.
Kaplan alisema, haki za kikatiba za Ghailani zilikiukwa kwa sababu Abebe alitajwa kutokana na taarifa aliyotoa Ghailani alipokua anateswa wakati anashikiliwa na Idara ya Ujasusi ya Marekani CIA.
Wachambuzi wanasema uwamuzi huu mahakimu ni pigo kubwa kwa utawala wa Rais Barack Obama na ahadi yake ya kuwafungulia mashtaka washukiwa wote wa ugaidi wanaoshikiliwa katika gereza la Guantanamo, katika mahakama ya kiraia.