Uhuru amechukuwa hatua hiyo baada ya kile alichosema kuwa ni kilio cha Wakenya kutokana na bei ya juu ya mafuta inayo sababisha kuongezeka kwa gharama ya maisha.
Katika hotuba yake kwa taifa Ijumaa kutoka ikulu ya rais, Nairobi, Kenyatta amesema kwamba anatarajia tume ya kudhibiti bei ya nishati Kenya, ERC, kupunguza bei ya mafuta ya petroli kutoka shilingi 127 hadi shilingi 118 na bei ya diseli kupungua kutoka shilingi 115 hadi shilingi 107.
“Siku chache zilizopita nimekuwa nikisikiliza maoni ya Wakenya na ni Dhahiri kwamba wana wasiwasi kuhusu kuongezeka gharama ya maisha inayoendeleakupanda,” amesema rais Kenyatta.
Hotuba ya Kenyatta inajiri saa chache baada ya kukataa kusainisheria ya fedha ya mwaka 2018 Alhamisi jioni na kurudisha muswada huo bungeni kwa marekebisho.
“Ni dhahiri kwamba nyote mmetatizwa na athari zinazoletwa na ushuru kwa bidhaa za mafuta ikiwemo kupanda kwa gharama ya maisha. Hivyo, nimewasikia na kuwaelewa,” amesema Kenyatta. Akiagiza wafanyabishara kushusha bei ya bidhaa, iliyokuwa imepanda, mara moja.
Kenyatta pia amependekeza kukata matumizi ya serikali kwa kupunguza safari za nje ya nchi, mikutano, mapokezi na burudani.
Kadhalika amependekeza kuongezwa fedha kwa idara za utekelezaji wa sheria kama ya msimamizi wa mashtaka na mahakama, ili kuweza kukusanya mapato zaidi kupitia mahakama nchini na kuimarisha uchunguzi utakaopelekea kuziba mwanya wa wizi wa fedha za serikali. Vile vile, amependekeza punguzo la matumizi ya fedha katika idara zote za serikali.
“Bado tuna tatizo la kufadhili bajeti yetu na kupunguza ushuru wa mafuta pekee sio suluhu kwa matatizo ya bajeti tuliyo nayo, wala haiwezi kusawazisha bajeti yetu inavyohitajika kisheria” amesema Kenyatta.
Rais Uhuru ameeleza kwamba serikali yake bado ina upungufu katika bajeti na ndio sababu amependekeza hatua za kubana matumizi katika idara zote za serikali, katika mapendekezo hayo yanayosubiri idhini ya bunge.
Spika wa bunge la taifa Justin Muturi ameitisha kikao maalum cha wabunge Jumanne na Alhamisi wiki ijayo kujadili muswada huo na kuufanyia marekebisho.
Wabunge wanatarajiwa kujadili mwelekeo wa Rais Kenyatta kuhusu sheria ya fedha ya mwaka 2018, inayopendekeza ushuru wa asilimia 8 badala ya asilimia 16.
Mapendekezo ambayo yamekataliwa na Kenyatta, yalipendekeza ushuru wa asilia 16, kusogezwa mbele kwa miaka miwili Zaidi, na kuanza kutumika mwaka 2020.
Sheria ya fedha ya kodi ya asilimia 16, iliidhinishwa na bunge mwaka 2013, ikiwa na lengo la kukusanya takriban dola milioni 340 kila mwala ili kuziba pengo la bajeti ya taifa na kupunguza deni la taifa kulingana na masharti ya shirika la fedha duniani, IMF.
Licha ya kuidhinishwa mwaka 2013, wizara ya fedha ilisimaisha utekelezaji wake mnamo mwaka 2016, na kuahidi kuitekeleza Septemba 1,2018. Deni la Kenya linakadiriwa kufikia asilimia 57.1 ya pato la taifa.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, VOA, Washington, DC.