Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 16:27

Kenya yasitisha kwa muda mpango wa kupeleka polisi Haiti


Maafisa wa polisi nchini Kenya.
Maafisa wa polisi nchini Kenya.

Kenya imeamua kusitisha mipango ya kutuma maafisa wa polisi nchini Haiti iliyokumbwa na ghasia chini ya ujumbe wa kimataifa unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, afisa mmoja mwandamizi wa serikali ya taifa hilo la Afrika Mashariki alisema Jumanne.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry kukubali kujiuzulu, huku magenge yenye silaha yakichukua udhibiti wa sehemu kubwa ya taifa hilo la Caribbean.

"Kumekuwa na mabadiliko ya kimsingi ya hali ilivyo kama matokeo ya kuvurugika kabisa kwa utaratibu wa sheria na kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa Haiti," Korir Sing'oei, katibu mkuu wa maswala ya kigeni, aliiambia AFP.

"Bila ya utawala wa kisiasa nchini Haiti, hakuna nanga ambayo kikosi cha polisi kinaweza kushikilia, na kwa hivyo serikali itasubiri kuanzishwa kwa mamlaka mpya ya kikatiba nchini Haiti, kabla ya kuchukua maamuzi zaidi kuhusu suala hilo," alisema.

Sing'oei alisema hata hivyo kwamba Kenya inasalia ikiwa imejitolea "kutoa uongozi kwa MSS," akimaanisha ujumbe wa Msaada wa Usalama wa Kimataifa ambao uliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Oktoba mwaka jana.

Katika wiki za hivi majuzi mzozo umekua mkali zaidi, huku miili ikitapakaa barabarani, majambazi wenye silaha wakipora miundombinu ya kimsingi na hofu ya kuongezeka kwa njaa ikiendelea kuwepo.

Kenya imesema ilikuwa tayari kupeleka hadi maafisa 1,000 nchini Haiti, lakini mipango hiyo imekabiliwa na changamoto za kisheria.

Akizungumza baada ya tangazo hilo la Kenya, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Matthew Miller aliwaambia waandishi wa habari: "Tutakuwa na wasiwasi bila shaka kuhusu ucheleweshaji wowote (wa kutumwa), lakini hatufikirii kwamba kutahitaji kucheleweshwa.

"Ukiangalia kile ambacho serikali ya Kenya ilisema katika taarifa yake ni kwamba wanapaswa kuwa na serikali ambayo watashirikiana nayo, ambayo imekuwa sehemu muhimu ya uelewa wao. Ni jambo la kawaida kabisa kutarajia," aliongeza.

Henry alikubali kujiuzulu Jumatatu wakati wa mkutano wa dharura wa Jumuia ya Mataifa ya Caribbean nchini Jamaica, ambako Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliahidi msaada wa ziada wa zaidi ya dola milioni 100 kuwezesha kupelekwa kikosi cha kimataifa nchini humo.

Akizungumza kutokea Pueto Rico, Waziri Mkuu Ariel Henry amesema kufuatia mkutano wa mawaziri wa Jumuia ya Mataifa ya Caribbean CARICOM, ameamua kujiuzulu akisema Haiti inahitaji amani, utulivu na maendeleo.

Henry “Serikali ninayoiongoza itaondoka mara tu baada ya kuundwa kwa baraza la utawala. Itaendelea kufanya kazi za siku hadi siku hadi pale waziri mkuu na serikali mpya itakapoteuliwa.”

Uamuzi wa kujiuzulu kwa Henry ulitangazwa na Rais Mohamed Irfaan Ali wa Guyana, Rais wa sasa wa CARICOM, baada ya mazungumzo ya faragha ya saa kadhaa ya mawaziri wa mambo ya nje wa jumuiya hiyo yaliyohudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken.

Akizungumza kwenye mkutano huo wa Jamaica Blinken amesema kutokana na ghasia za magenge ya uhalifu kupata nguvu inadhihirisha umuhimu mkubwa wa kupelekwa kwa kikosi cha kimataifa.

Blinken amesema “kutokana na hali ya dharura inayojitokeza ninatangaza hii leo kwamba Wizara ya Ulinzi ya Marekani inaongeza maradufu msaada wake kwa kikosi hicho kutoka dola milioni 100 kufikia dola milioni 200, na hivyo kwa ujumla inafikisha msaada wa Marekani kuwa milioni 300 kwa ajili ya juhudi hiyo.

Zaidi ya hapo ninatangaza msaada wa dharura wa dola milioni 33 kusaidia huduma za afya na chakula za Haiti.”

Hata hivyo haifahamiki bado jinsi utawala wa mpito utakavyo undwa na wachambuzi wanasema haikowazi iwapo mipango hiyo ya kimataifa itaweza kutekelezwa kwani wakuu ya magenge ya uhalifu wanataka kuhusishwa kwenye utaratibu kamili.

Kiongozi wa magenge hayo Jimmy Cherizer anayejulikana kama “Barbacue” akizungumza na waandishi habari mjini Port au Prince amesema wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwapatia Wahaiti nafasi ya kujiamulia mustakbali wao.

Cherizer ‘Barbacue’ anaeleza “tunacho omba ni kuchaguliwa mtu atakaye ongoza nchi anayeishi pamoja na sisi na uamuzi kufanywa na wananchi wa Haiti. Tunataka mawaziri wote watoke katika jamii ya wahaiti.”

Haiti hivi sasa iko katika hali ya dharura tangu Machi 3 na Barbecue amewaonya wamiliki wa hoteli kuu zote kuhakikisha hawapapi hifadhi mawaziri wa serikali na kwamba watavamia hoteli moja hadi nyingine kuhakikisha jambo hilo halifanyiki.

Forum

XS
SM
MD
LG