Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 15:34

Katika ujumbe wa Pasaka, Papa Francis atoa wito wa sitisho la vita vya Gaza


Papa Francis wakati wa misa ya Pasaka 2024.
Papa Francis wakati wa misa ya Pasaka 2024.

Kiongozi mkuu wa kanisa katoliki Papa Francis alitoa wito wa sitisho la mapigano la mara moja katika mzozo kati ya Israel na Hamas huko Gaza, wakati Wakristo duniani kote wakisherekea siku kuu ya Pasaka Jumapili.

Hayo yalijiri huku nayo mashirika ya misaada yakisumbuka kufikisha misaada katika maeneo yanayokaliwa ya Wapalestina.

Mbele ya umati uliofurika kwenye uwanja wa Mtakatifu Petro uliojaa maua, Papa Francis alitoa ujumbe wa amani huko Gaza.

“Ninatoa wito kwa mara nyingine tena kwamba upelekaji wa misaada ya kibinadamu uhakikishwe huko Gaza na ninatoa wito kwa mara nyingine tena kuachiliwa kwa haraka kwa mateka waliokamatwa tarehe 7 Oktoba na kusitisha mapigano mara moja katika Ukanda wa Gaza. Tusiruhusu uhasama uliopo kuendelea kusababisha madhara makubwa kwa raia haswa kwa watoto,” alisema.

Wito wa kupeleka misaada huko Gaza uliongezeka katika siku za hivi karibuni, huku misafara ya meli ikiondoka kwenye bandari ya Cyprus Jumamosi ikibeba tani 400 za chakula na vifaa vingine vya misaada.

Shirika la World Central Kitchen linasema meli hizo zimebeba vyakula ambavyo viko tayari kuliwa kama vile mchele, pasta, unga, mboga za makopo na protini, kutosha kuandaa milo zaidi ya milioni 1.

Umoja wa mataifa unaonya kwamba eneo la kaskazini mwa Gaza linaweza kukumbwa na njaa kuanzia mwezi Machi

Jeshi la Marekani, pamoja na washirika wengine wa kikanda, linaendelea kudondosha kwa ndege chakula na maji.

Lakini usambazaji huo wa misaada unaweza kutokuwa na manufaa ikiwa hakuna njia yoyote iliyopangwa ya kufanya usambazaji wa ardhini.

Israel ilitangaza vita dhidi ya Hamas kufuatia shambulio la Oktoba 7 lililofanywa na kundi hilo la wanamgambo ambalo liliua watu 1,200 na kuteka nyara zaidi ya wengine 250.

Tangu wakati huo Israel imeweka vikwazo kwenye eneo lote, ikishambulia majengo ya raia na kuzuia misaada kuingia kwa wingi.

Maafisa wa afya huko Gaza wanasema zaidi ya Wapalestina 32,000 wameuawa.

Mahakama ya sheria ya Umoja wa mataifa ilichukua hatua mbili za muda katika kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini ikiishtumu Israel kufanya mauaji ya kimbari, mashtaka ambayo Israel inayakanusha vikali.

Lakini kwa Waisraeli wengi, vita vinavyoendelea sio suluhisho, huku wakiandamana barabarani wakiitaka serikali yao kusaini makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas kwa ubadilishanaji wa mateka ambao bado wanashikiliwa na kundi hilo linalochukuliwa na mataifa ya magharibi kama kundi la kigaidi.

Jumapili, kwenye kanisa la Holy Sepulcher mjini Jerusalem, ambalo linachukuliwa na Wakristu kama mahali patakatifu

zaidi, askofu mkuu alisimamia misa ya Pasaka katika kanisa ambalo lilikuwa tupu ikilinganishwa na miaka iliyopita, kwa sababu tangu Oktoba 7, waumini wa Kipalestina wanahitaji ruhusa maalumu ya kuvuka vituo vya ukaguzi ili kuingia Jerusalem.

Forum

XS
SM
MD
LG