Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 21:34

IGP akanusha kupata taarifa za kutishiwa Lissu usalama wake


Mbunge wa Chadema Tundu Lissu
Mbunge wa Chadema Tundu Lissu

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limesema kuwa Mwanasheria Mkuu wa Chadema Tundu Lissu hajawahi kutoa taarifa katika chombo chochote cha ulinzi na usalama kwamba anafuatiliwa na watu wasiojulikana.

Kauli hiyo aliitoa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, Ijumaa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusiana na shambulizi la risasi lilomjeruhi Lissu.

Kwa sababu Lissu alikuwa hajatoa taarifa hatua hiyo imelifanya jeshi la polisi lishindwe kujua kinachoendelea dhidi yake, alisema Sirro.

Lakini hivi karibuni, Lissu, alitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwamba alikuwa anafuatiliwa kwa wiki tatu na vijana wasiojulikana wanaotumia gari aina ya Toyota Premio, yenye namba za usajili T460 CQV na aliwazuia karibu na Kanisa la Mtakatifu Petro la Oysterbay, Dar es Salaam.

Hata hivyo Sirro ameendelea kusisitiza kuwa: “Lissu hajawahi kutoa taarifa za kufuatiliwa na watu wasiojulikana, mambo haya ndio kwanza tunasikia leo (Ijumaa), yawezekana alikuwa akizungumza kisiasa, tunamuomba Mungu amponye ili aweze kutuambia suala hilo tutakaloweza kulifanyia kazi,” alisema.

Katika maelezo yake, IGP ameeleza kuwa risasi zilizomjeruhi Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, zilirushwa kutoka bunduki aina ya SMG, zinazotumiwa na wahalifu wengi.

Sirro alisema silaha hizo zimekuwa zikiingizwa nchini na wahalifu kwa njia mbalimbali, jambo ambalo ni rahisi kupatikana.

IGP Sirro amesema kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limeunda timu ya wapelelezi waliobobea kutoka Makao Makuu ya Dar es Salaam na wamekwenda mkoani Dodoma ili kufuatilia tukio hilo na kusaidia kupatikana ukweli wake.

“Tumetuma wapelelezi waliobobea kwenda mkoani Dodoma kwa ajili ya kufuatilia suala hilo, hivyo basi tunaamini wahusika wa shambulizi hilo tutawapata na kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema.</p>

Sirro alisema timu hiyo imekwenda kuongeza nguvu kwa askari waliopo mkoani humo, ambao tayari wameanza kufuatilia suala hilo tangu lilipotokea.

Pia alisema jeshi hilo linafuatilia wananchi waliokuwa wakitoa taarifa kwenye mitandao ya kijamii ili waweze kuisaidia polisi katika tukio hilo.

Alisema kwa sasa wanafuatilia taarifa hizo wanazoamini zinaweza kuwasaidia kwenye uchunguzi wao.


XS
SM
MD
LG