Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 19:35

Kenyatta : Mafanikio ya ugatuzi Kenya ni 'hatua ya kihistoria'


Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta amesema ametekeleza Katiba ya Kenya ya 2010 na ameufanya ugatuzi kuwa ni suala linalo wezekana.

Rais ameainisha, katika hotuba yake ya hali ya taifa, mafanikio ya serikali yake kwa kipindi cha miaka minne katika maeneo ya usalama wa taifa, utulivu wa eneo la Afrika Mashariki, kukasimu madaraka kwenye serikali za kaunti, uchumi, elimu, na afya kati ya mambo mengine.

Ugatuzi

Kuhusu ugatuzi, Kenyatta amesema, katika hotuba yake ya mwisho alioitoa Jumatano, Kenya ilikuwa imepiga hatua kubwa, akielezea kukasimu madaraka na mgao wa fedha ambao umefanywa na serikali yake kama ni “hatua ya kihistoria” ambayo serikali chache duniani zinafuata mfumo huo.

Rais amesema kuwa uongozi wake umekwenda mbali zaidi ya kile kinachotakiwa na katiba kwa kuongeza kiwango cha mgao wa mapato katika kaunti hizo kutoka asilimia 15 kufikia 34 ya pato la taifa.

Mikopo yenye masharti

Uongozi wake, amesema, ulikuwa umezisaidia serikali za kaunti kupitia mikopo yenye masharti kuboresha nyanja za afya na maji.

“Msaada wetu katika ugatuzi umetusukuma kutafuta na kutekeleza, kwa kushirikiana na kaunti, miradi ambayo inaathari chanya kwa wakazi wa kaunti hizo.

Kiongozi huyo wa taifa amesema serikali ya Jubilee imeongeza kasi kukasimu madaraka, fedha na wafanyakazi kutoka katika ngazi za kitaifa kwenda kwenye maeneo ya ugatuzi 47.

Kutokomeza ugaidi

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa miongoni mwa mafanikio hayo ni kuweka mikakati thabiti kutokomeza ugaidi.

Aidha, Bwana Kenyatta pia amegusia mafanikio katika kukabiliana na hali hiyo ya uvunjifu wa amani unaotokana na ugaidi na ukame, mambo ambayo yamekuwa yakiwaathiri Wakenya wengi.

Lakini wachambuzi wa siasa nchini Kenya wanasema kuwa kwa miaka minne akiwa madarakani Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akikabiliwa na shutma mbalimbali kutokana na kuyumba kwa hali ya usalama nchini.

Pia kumekuwa na malalamiko kuhusu kuongezeka kwa ripoti za ufujaji wa mabilioni ya fedha katika wizara mbalimbali.

Mafanikio ya serikali

Hata hivyo katika hotuba yake, Bwana Kenyatta ameeleza kuwa serikali yake imepata mafanikio mkubwa mno ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika serikali zilizokuwa madarakani.

Wakati huohuo Rais amewarai Wakenya kumchagua mara nyingine ili serikali yake irudi madarakani kwa awamu nyingine ya miaka mitano,

Kenyatta ameendelea kusema kuwa serikali yake itaendelea kupambana na uhalifu na uvunjaji wa sheria ikiwa ni pamoja na ujangili na migogoro baina ya jamii za wafugaji.

Ukame nchini Kenya

Kufuatia upungufu wa mvua, ukame umeendelea kuathiri zaidi ya Wakenya milioni mbili kutoka kaunti zaidi ya kumi na mbili na hata kuwepo kwa ripoti kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka na kuongeza baa la njaa.

Rais Kenyatta amewataka viongozi wa serikali za kaunti kushirikiana na serikali kuu kudhibiti janga hilo.

“Nakubali hali ya ukame inayoendelea imeathiri kwa kiwango kikubwa sehemu kubwa ya watu wetu na hasa jamii za wafugaji ambao mifugo yao inakosa malisho na maji,” rais amesema.

“Ni jukumu la viongozi wetu, katika ngazi zote, washirikiane na uongozi wa kitaifa kuhakikisha kuwa majimbo yao yanapata misaada ya kujikimu kutokana na ukame inayotolewa na serikali, ikiwemo programu ya kuinusuru mifugo yao.

Tishio la al-Shabaab

Aidha, Rais Kenyatta ametambua kuwa usalama wa nchi umekuwa ukididimizwa na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na kundi la kigaidi la al-Shabaab ambalo tangu aliposhika hatamu za uongozi lilikuwa likivuka mipaka ya nchi na kufanya mashambulizi.

Kenyatta anaeleza kuwa jitihada za serikali yake kuzuia mitandao inayotoa mafunzo ya itikadi kali pamoja na kupeleka majeshi ya Kenya kujiunga na Amisom zimeonyesha mafanikio.

Rais Kenyatta pia amekiri kuwa serikali yake imekuwa ikitumia shilingi bilioni 627 kwa mahitaji ya umma ambayo ni asilimia hamsini ya mapato ya jumla ya serikali. Fedha ambazo zinazotumika kulipa mishahara na marupurupu ya wafanyakazi wa umma.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya.

XS
SM
MD
LG