Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 20:05

Mgomo wa Madaktari wamalizika Kenya


Madaktari Kenya
Madaktari Kenya

Hatimaye madaktari wameamua kurudi kazini nchini Kenya, baada ya kusaini makubaliano ya pamoja na Serikali juu ya utaratibu mpya katika ajira zao.

Makubaliano hayo yamemaliza mgomo wa wafanyakazi ulioendelea kwa siku 100 na kuathiri maisha ya watu wengi nchini, gazeti la Daily Nation Kenya limeripoti.

Awali Wizara ya Afya na Magavana walifikia makubaliano kuhusu nyaraka ambazo zilikuwa ni pingamizi katika kumaliza mgomo wa madaktari uliodumu kwa muda mrefu.

Mawakili wa Baraza la Magavana na wizara ya afya waliwaambia majaji kuwa watapeleka mkataba wao wa makubaliano ya pamoja juu ya utaratibu wa kurudi kazini kwenye mahakama ya rufaa mchana wa Jumanne, vyanzo vya habari Kenya vimeeleza.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo madaktari pia walipeleka rasimu ya “formula” ya utaratibu wa kurejea kazini mahakamani siku ya Jumatatu,

Wakili Waigi Kamau wa wizara aliwahakikishia majaji Hannah Okwengu, Martha Koome na Jamilla Mohammed kuwa serikali iko katika mchakato wa kukamilisha “formula” ya utaratibu wa pamoja unaohusu madaktari kurejea kazini.

Kamau alisema serikali haina tatizo na rasimu hiyo iliyoletwa na madaktari na kuwa makubaliano ya pamoja yatafikishwa mahakamani mara baada ya pande zote kusaini.

Majaji wamezipongeza pande zote mbili kwa kufikia makubaliano juu ya waraka huo ambao ulikuwa sababu ya kusimama shughuli zote katika hospitali za umma.

XS
SM
MD
LG