Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 08:02

Hatimaye Sudan Kusini yaunda serikali ya umoja wa taifa


Riek Machar na Salva Kiir Mayardit wakizungumza na waandishi wa habari Juba, Sudan Kusini Februari 20, 2020. REUTERS/Jok Solomun
Riek Machar na Salva Kiir Mayardit wakizungumza na waandishi wa habari Juba, Sudan Kusini Februari 20, 2020. REUTERS/Jok Solomun

Rais wa Sudan Kusini amechukua hatua ya kihistoria iliyokuwa inasubiriwa kwa muda mrefu kwa kulivunja baraza la mawaziri na kumchagua kiongozi wa upinzani Riek Machar kuwa makamu wa kwanza wa rais, siku moja kabla ya kuapishwa Jumamosi kwa serikali ya mpito ya umoja wa taifa.

Katika amri ya kiutendaji ya rais iliyotangazwa Ijumaa katika vyombo vya habari vya Sudan Kusini, Salva Kiir pia alimteua Rebecca Nyandeng, mjane wa mwanzilishi wa taifa hilo John Garang, kuwa moja kati ya makamu wa rais watano, akiwemo Machar, Wani Igga, taban Deng Gai, na mtu mmoja zaidi ambaye bado hajatajwa.

Kiir pia ametoa amri ya kiutendaji kuvunja baraza la mawaziri na jopo la washauri wake. Amemchagua Tut Gatluak Kew kuwa mshauri wa rais juu ya masuala ya kiusalama na Mayik Ayii Deng kuwa waziri katika ofisi ya rais.

Mgawanyiko wa kikabila na mvutano wa kisiasa kati ya Kiir na Machar ulianzisha vita ya wenyewe kwa wenyewe Sudan Kusini Disemba, 2013.

Vita hivyo vilisababisha wananchi milioni 4 wa Sudan Kusini kukimbia makazi yao na maelfu zaidi kupoteza maisha kutokana na mapigano, njaa na maradhi.

Vyanzo vya habari nchini Sudan Kusini vimeeleza Riek Machar aliapishwa kuwa makamu wa rais, muundo ambao ulishindwa kufanya kazi mara mbili na kuitumbukiza nchi hiyo kwenye mzozo wa vita uliowauwa karibu watu 400,000.

Sudan Kusini, taifa changa kabisa duniani lilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe 2013 baada ya wafuasi wa Kiir na Machar kushindwa kuelewana baada ya nchi hiyo ilipofanikiwa kupata uhuru wake kutoka Sudan.

Mnamo mwaka 2018 mikakati iliowekwa na jumuiya ya kimataifa iliwezesha taifa hilo kufikia makubaliano ya amani.

Kwa upande wake kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis alionyesha unyenyekevu mkubwa katika juhudi zake za kutafuta suluhisho la kudumu Sudan Kusini na alikutana na mahasimu hao wawili Kiir na Machar na kuibusu miguu yao huku akiwanasihi wamalize uhasama wakati walipomtembelea mjini Vatican mwaka uliopita.

Sherehe za kuundwa serikali mpya mjini Juba zilianza kwa viongozi hao kukabidhiwa picha ya tukio hilo ili iwe ukumbusho wa wajibu waliokuwa nao.

XS
SM
MD
LG