Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 19:23

Dunia yaadhimisha siku ya wanawake kwa wito wa usawa, mabadiliko


Wanawake wakiwa na mabango yao juu wamekusanyika nje ya Bunge la Ulaya wakipinga uonevu dhidi ya tofauti ya mishahara baina yao na wanaume, uvunjifu wa amani na kukosekana haki katika maeneo mengi, mjini Brussels, Ijumaa, Machi 8, 2019.
Wanawake wakiwa na mabango yao juu wamekusanyika nje ya Bunge la Ulaya wakipinga uonevu dhidi ya tofauti ya mishahara baina yao na wanaume, uvunjifu wa amani na kukosekana haki katika maeneo mengi, mjini Brussels, Ijumaa, Machi 8, 2019.

Afrika Mashariki na kila pembe ya dunia sherehe za siku ya wanawake zimefanyika ambapo kumekuwepo na maandamano, mikutano na wito wa kuwepo usawa na ubunifu katika kuleta mabadiliko ya wanawake.

Kwa upande wa Tanzania imeungana na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha siku ya wanawake duniani.
Umoja wa mataifa ulitangaza kila Machi 8 kuwa ya maadhimisho siku ya wanawake duniani kusheherekea mchango wa wanawake katika maendeleo pamoja na kuangazia na kuendeleza haki za wanawake katika jamii.
Hatua hiyo ni kutoa chachu ya kuleta usawa wa kijinsia na maendeleo pamoja na kutokomeza kila aina ya ubaguzi, vitendo vya udhalilishaji na ukatili dhidi ya wanawake.
Hapa nchini maadhimisho hayo mwaka huu yanafanyika katika kila mkoa yakiambatana na shughuli mbalimbali yakiwa na kauli mbiu isemayo 'Badili Fikra, Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu"
Akizungumzia maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Julius Mbilinyi ametoa wito kwa wanawake kujitokeza kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali katika kuhakikisha maendeleo endelevu.

UN

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amesema usawa wa jinsia na haki za wanawake ni msingi wa maendeleo duniani.

Ethiopia

Huko Ethopia shirika la ndege la Ethopia Airlines limeadhimisha siku hii kwa kuandaa safari ya ndege kutoka Addis Ababa hadi Oslo iliyosimamiwa na wanawake pekee yao kuanzia marubani hadi wafanyakazi wote ndani ya ndege hiyo.

Ufaransa

Huko Paris shirika la haki za binadamu la Amnesty International liliandaa mkusanyiko mbele ya ubalozi wa Saudi Arabia kutowa wito wa kufunguliwa wanawake watatu wanaharakati wa haki za binadamu wa Saudi Arabia walio kizuizini bila ya kufunguliwa mashtaka.

Brussels

Wanawake pia wakiwa wamenyanyua mabango yao juu wamekusanyika nje ya Bunge la Ulaya wakiadhimisha siku hii, wakipinga uonevu dhidi ya tofauti ya mishahara baina yao na wanaume, uvunjifu wa amani na kukosekana haki katika maeneo mengi.

Korea Kusini

Katika mji mkuu wa Korea Kusini wa Seoul wanawake walikusanyika kuzungumzia changamoto zinazowaathiri na suluhisho kwa ubaguzi wa kijinsia na namna ya kupambana na unyanyasaji huo wa kingono.

Ufilipino

Maandamano yalifanyika pia huko Ufilipino dhidi ya rais wao Rodrigo Duterte kwa kuwadhalilisha wanawake, na kutoa usawa wa kijinsia.

Sherehe za mwaka huu zimefanyika wakati kuna wanawake wengi walofanikiwa kuingia katika jukwa la kisiasa katika maeneo mbali mbali ya dunia.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Abdushakur Aboud, Washington, DC

XS
SM
MD
LG