Hapa Marekani sherehe za kitaifa zinafanyika katika makaburi ya Arlington, katika njia ya kipekee kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19 wakati Wamarekani wakisherekea siku ya mashujaa.
Sherehe mbali mbali duniani zinafanyika leo kuwakumbuka wanajeshi takriban milioni tisa waliofariki katika vita vya kwanza duniani kati ya mwaka 1914 hadi 1918.
Huko Ufaransa Rais Emmanuel Macron aliweka shada la maua kwenye mnara wa Arc de Triomphe mjini Paris bila ya wananchi kuhudhuria kutokana na janga la virusi vya corona.
Wakati huo huo kundi la wanajeshi wa Ufaransa wamemaliza mbio za kupokezana za siku 5 kwa kukimbia km 360, kutoka mji wa Verdun hadi Paris. Walikimbia kupitia njia ambayo maiti ya waanajeshi wawili ambao hawakujulikana majina yao mmoja ni Mfaransa na mmoja Uingereza, zilisafirishwa miaka 100 iliyopita kuwakumbuka wanajeshi waliouwawa bila ya kujulikana ni kina nani wakati wa vita hivyo.
Mtayarishaji wa mbio hizo za kupokezana mwenge Kanali Thibault de Brebison anaeleza lengo la mbio hizo : Lengo la mbio hizi kubeba mwenge kutoka Verdun hadi Paris ni kutoa heshima kwa wote waliofariki na kuonyesha kwamba Novemba 11 sio siku ya waliofariki kwenye vita vya kwanza vya dunia bali watu wetu wote waliofariki. Na hii leo hasa ni kuwakumbuka pia waliofariki mwaka 2020.
Huko Korea Kusini katika makaburi ya makumbusho ya wanajeshi wa Umoja wa Maifa mjini Busan sherehe zimefanyika kuwakumbuka wanajeshi wa umoja huo waliouawa kwenye vita vya Korea. Na leo imetangazwa rasmi mjini huko kuwa siku ya kimataifa ya makumbusho ya mashujaa wa vita vya Korea.
Waziri Mkuu wa Korea Kusini Chung Sye-Kyun amesema mnamo miaka 70 tangu kumalizika vita hivyo Korea Kusini imeendelea kutoka taifa maskini hadi kuwa miongoni mwa mataifa 10 tajiri duniani. Na kuonegza kusema kwa nguvu inabidi kuendeleza juhudi za kupatikana amani.
Chung Sye-kyun, Waziri Mkuu wa Korea Kusini anasema : "Tutaendelea na juhudi za kuwepo majadiliano ili kupata amani ya kudumu kwenye Peninsula ya Korea ambayo itazingatia juu ya ulinzi thabiti wa kitaifa."
Kutokana na janga la virusi vya corona sherehe za mwaka huu katika nchi nyingi zinafanyika bila ya magwaride ya kijeshi kuwakumbuka waliofariki, bali maafisa wa serikali wanaweka mashada ya maua kwenye makaburi ya wanajeshi wasiojulikana.