Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 15, 2025 Local time: 09:59

Couscous chakula cha nchi za Afrika Kaskazini chatambuliwa na UNESCO


Wanawake wa Ki-Berber Algeria watayarisha Couscous kuadhimisha mwaka mpya kijijini Ait el-Kecem
Wanawake wa Ki-Berber Algeria watayarisha Couscous kuadhimisha mwaka mpya kijijini Ait el-Kecem

Couscous, chakula cha watu wa kabila la Berber, wanaopatikana Afrika ya Kaskazini kimekuwa maaurufu sana katika kanda hiyo na kwengineko duniani.

Hivi karibuni kimetambuliwa na kuwekwa kwenye orodha ya urathi wa utamaduni ya Shirika la Umoja wa Mataifa, la Sayansi na Utamduni Unesco. Kinatambuliwa hivi sasa kama urathi wa kiutamaduni duniani.

Mataifa yaliyo wasilisha pendekezo ili chakula hicho kiwekwe kwenye orodha ya UNESCO ni pamoja na Algeria, Morocco, Tunisia na Mauritania huenda yakawa na tofauti kubwa kati yao, lakini upendo wao wa nafaka hiyo ya Couscous pengine ndio inawaunganisha pamoja.

Mpishi Mmorocco atayarisha mloo wa Couscous katika mgahawa mjini Rabat
Mpishi Mmorocco atayarisha mloo wa Couscous katika mgahawa mjini Rabat

Pendekezo lililowasilishwa kwa pamoja na nchi hizo nne kwa baraza la Unesco, lilitoa hoja kwamba Couscous, haikosekani katika kila shughuli aidha ya kitamaduni au kijamii, hivyo kwa wakati mmoja ni chakula cha kawaida na spesheli. Wanaeleza kuwa Couscous si chakula tu cha kawaida kwa sababu kinaliwa sana, lakini ni spesheli kwa kuwa kina kuwa na jukumu maalum la kuunganisha watu kwenye mijumuiiko ya kijamii ambapo chakula huletwa na kuliwa.

Nafaka hiyo ya Couscous, ikiliwa peke yake, haina mvutio sana, lakini pale unapoata kitoweo cha samaki au nyama, na michuzi na mboga zenye ladha, basi Couscous huwa chakula kitamu kweli. Kila nchi kati ya hizo nne zinajivunia kuwa na Couscous bora zaidi kuliko mwngine.

Na hivyo Mpishi kutoka Tunisia Taeib Bouhadra, anasema nchi yake inajivunia sana upishi wake tofauti tofauti wa Couscous, akisema wana aina nyingi ya nafaka hio na takriban kila nyumba ina aina yake.

Taeib Bouhadra Mpishi kutoka Tunisia anasema : “Ni chakula kizuri sana. Na kinaokana na watu wa kabila la Berber. Wao ni wa kwanza katika kanda ya Maghreb ya Afrika yaani, nchi za Tunisia, Morocco, Algeria na Libya. Lakini Coucous bora zaidi, ni ile kutoka Tunisia, hata kwenye mashindano tulioshiriki na Morocco na Algeria, Couscous ya Tunisia imeshinda tuzo nyingi.”

Mgombea kiti cha Meya wa Paris Nathalie Kosciusko-Morizet akipakua Couscous wakati wa kampeni
Mgombea kiti cha Meya wa Paris Nathalie Kosciusko-Morizet akipakua Couscous wakati wa kampeni

Kote katika kanda ya Maghreb, Couscous pia inajulikana kama Seksu, au Kusksi au Kseksu, ni chakula kikuu kama vile mchele au tambi zilivyo kwa watu wa Asia, au Ugali kwa watu wa Afrika mashariki, basi Couscous nayo, haikosekani kwenye nyumba ya watu wa nchi za Afrika Kaskazini.

Katika kamusi za kiarabu, nafaka hiyo ya Couscous iliorodheshwa tangu Karne ya 19, japo inajulikana kuwa ilikuwepo hata kabla ya hapo.

Bahoudra anaamini kuwa Couscous ilionekana kwanza kwenye milima ya Atlas katika mwaka 218 kabla kuzaliwa kwa yesu, na sasa inauzwa duniani kote.

Taeib Bouhadra: “Couscous inauzwa kote duniani na huwa nasema kuwa Couscous imekuwa chakula kikubwa kuliko hata pasta. Leo kuna hata mashindano ya dunia ya Couscous huko Sicily Italy. Ni shindano ambalo hushirikisha zaidi ya mataifa kumi. Hata Brazil kuna mashindano ya kupika Couscous”

Mmiliki wa mgahawa kutoka Morocco, Hicham Hazzoum alikuwa miongoni mwa wapishi wa kwanza wa Couscous waliofurahia tuzo hiyo ya hadhi ya Couscous kutoka Unseco.

Hazzoum asema : “Nadhani muda umefika kwa Couscous ya Morocco kutambuliwa duniani kote, kama vile Pizza na mapishi mengine yanavyotambuliwa. Lakini ukilinganisha ubora wake, hauwezi kulinganisha. Kwa hiyo ninawashukuru wale walioipatia nafaka hii utamubulisho huu, pamoja na kuchelewa kutambulika, thamamni yake, lakini nafaka hii inastahiki kutambuliwa huko na Unesco.”

Sufuria kubwa ya kupikia couscous kwa mvuke iliyochongwa kwa bati na kuwekwa Kairouan Tunisia
Sufuria kubwa ya kupikia couscous kwa mvuke iliyochongwa kwa bati na kuwekwa Kairouan Tunisia

Couscous hutayarishwa kutokana na ngano au shyiri. Na mara nyengine pia kutoka mahindi, au mtama, ambayo husagwa na kuwa semolina.

Hii kisha hufanywa kama tembe ndogo, ambayo huchujwa na baadae kuloekwa majini na kisha kupikwa kwa mvuke.

Wanawake hususan huwa na jukumu kubwa katika utengenezaji na upishi wa Couscous.

Wasichana nao sio tu hujifunza kupika Couscous, lakini pia wanajifunza mbinu zote za utengenezaji wa nafaka hio na hata nyimbo zinazoimbwa wakati wa mchakato mzima wa utayarishaji wa Couscous kuanzia uzalishaji hadi upishi.

Katika kanda lenye mgawanyiko, kuna matumaini kuwa kutambuliwa Couscous na Unesco kutaboresha hali na hadhi ya umoja wao.

Pendekezo la Couscous lafikishwa Baraza la UNESCO
please wait

No media source currently available

0:00 0:04:09 0:00
XS
SM
MD
LG