Hiyo ni kufuatia Beijing kukata mawasiliano na Washington ikilipiza kisasi kufuatia ziara ya Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi huko Taiwan mapema wiki hii.
Blinken alizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kwa njia ya mtandao na mwenzake wa Ufilipino huko mjini Manilla baada ya kukutana na Rais mpya aliyechaguliwa Ferdinand Marcos Jr. na viongozi wengine wa ngazi ya juu, wakati uhusiano kati ya Washington na Beijing ukiendelea kushuka kwa kiwango kibaya zaidi kwa miaka kadhaa.
Ziara ya Pelosi katika kisiwa kinachojitawala imeikasirisha China, inayodai kuwa Taiwan ni sehemu ya himaya yake na ikibidi itaichukua kwa nguvu. China siku ya Alhamisi ilianzisha mazoezi ya kijeshi nje ya pwani ya Taiwan na siku ya Ijumaa ilikata mawasiliano na Marekani katika masuala muhimu, ikiwemo masuala ya kijeshi na ushirikiano muhimu kuhusu hali ya hewa, kama adhabu kwa ziara ya Pelosi.
“Hakuna haja ya kuushikilia mateka ushirikiano katika mambo muhimu ya kimataifa kwa sababu ya tofauti zilizopo kati ya nchi zetu mbili,” Blinken alisema. “Wengine wanatarajia sisi tuendelee kushughulikia masuala yaliyo muhimu kwa maisha na mahitaji ya watu wao na pia watu wetu.”
Alielezea ushirikiano wa mabadiliko ya hali ya hewa kuwa ni eneo muhimu ambapo hatua ya China kukata mawasiliano “haiiadhibu Marekani – inaiadhibu dunia.”
“Mzalishaji mkubwa sana duniani wa hewa ya carbon hivi sasa anakataa kujihusisha katika kutatua mgogoro wa hali ya hewa,” Blinken alisema, akiongeza kuwa China inafyatua makombora ya ballistic ambayo yanatua katika maji yanayoizunguka Taiwan ni hatua hatari sana na inaweza kudumaza uthabiti.
China ilisitisha mawasiliano ya jeshi kwa jeshi, ambayo ni muhimu kuepusha kupoteza mawasiliano na kuepusha migogoro, lakini pia ushirikiano wa kukabiliana na uhalifu unaovuka mipakani na kupambana na madawa ya kulevya, ambapo inasaidia kuwafanya watu wa Marekani, China na nchi nyingine kuishi kwa salama,” alisema.
Chanzo cha habari hizi ni shirika la habari la AP.