Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken, Juatano ametoa kauli inayo tarajia kupunguza wasiwasi uliopo kuhusiana na eneo la Taiwan kwa kusema Marekani ni muumini wa sera ya China moja.
Kauli hiyo imetolewa wakati ambao kuna wasiwasi uliotanda mara baada ya kufanyika ziara ya spika wa baraza la wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi ambayo iliikasirisha Beijing.
Akiongea katika mkutano wa jumuiya ya mataifa ya kusini mashariki mwa Asia – ASEAN nchini Cambodia, waziri Blinken amesema kwamba “nataka kusisitiza kwamba hakuna kilicho badilika kuhusu msimamo wetu, na natarajia kwamba Beijing haitaanzisha mgogoro ama kutafakari kuongeza nguvu katika shughuli zake za kijeshi.”
Marekani imekuwa ikiongeza kasi ya uwepo wake na kujihusisha katika eneo la Asia na Pacific, ambapo waziri Blinken, kabla ya mkutano wa mawaziri wa ASEAN amesema kwamba Washington inatarajia kuongeza ushirika wake na jumuiya hiyo katika ukanda wake wote.