Hoja ya Wademokrats kutaka kuletwa mashahidi ilionekana kushindwa baada ya Warepublikan waliotarajiwa kuungana nao kubadili mawazo yao na hivyo wachambuzi wanasema huenda kesi ikamalizika Ijumaa usiku na kumfutia mashtaka rais Trump.
Seneta Mrepublikan Lamar Alexander, aliyetarajiwa kuleta mabadiliko kwenye kesi hiyo, alitangaza jana kwamba hataunga mkono hoja ya kuruhusu mashahidi na kuvuruga matumaini ya Wademokrats kupata wenzao watatu tu kufikia kura 51 zinazohitajika kuruhusu mashahidi na kesi kuendelea.
Hivi sasa zinahitajika theluthi mbili za kura katika Baraza la Seneti kumuondoa rais jambo ambalo halitawezekana na hivyo kuna uwezekano mkubwa hatopatikana na hatia na kesi kumalizika.
Wachambuzi hivi sasa wanasema Wademokrats wanataka kuhakikisha kwamba Trump hatachukuwa uamuzi huu kuwa ni ushindi kwani wamedhihirisha alifanya makosa.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.