“Ushirikiano wetu wa ulinzi dhidi ya Daesh ni nguzo muhimu ya uhusiano wetu wa pamoja, na Marekani bado ina nia ya dhati katika mapambano hayo kuisaidia Iraq katika ulinzi na usalama wa eneo zima,” Austin aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano wake na Waziri Mkuu wa Iraqi Mohammed Shia al-Sudani.
Austin aliwashukuru viongozi wa Iraq kwa ahadi yao ya kuhakikisha majeshi ya ushirika yanayofanya operesheni zake nchini Iraqi yatalindwa kutokana na hujuma ya “wasaliti wa ndani na nje ya nchi.”
Majeshi ya Marekani na Ubalozi wa Marekani mjini Baghdad wamekuwa ndiyo lengo la roketi zinazorushwa na wanamgambo wanaungwa mkono na Iran.
Marekani ina takriban wanajeshi 2,500 nchini Iraq ikiwa na jukumu la kushauri na kuyasaidia majeshi ya Iraqi katika vita vyake dhidi ya kikundi cha Islamic State.
Austin ameipongeza Iraq kuwarejesha raia wa Iraqi kutoka katika vituo vya vizuizi na kambi za watu wasiokuwa na makazi kaskazini mashariki mwa Syria na kuzishawishi nchi zote kufanya hivyo hivyo kwa raia wao.
Baadhi ya taarifa katika ripoti hii zinatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters