Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 15, 2025 Local time: 14:14

App yatumika kuwaelimisha wasichana Kenya kuhusu hedhi


Wasichana wakiwa na watoto wao nje ya bweni la shule ya sekondari ya Serene Haven huko Nyeri, Kenya. Picha na REUTERS/Monicah Mwangi.
Wasichana wakiwa na watoto wao nje ya bweni la shule ya sekondari ya Serene Haven huko Nyeri, Kenya. Picha na REUTERS/Monicah Mwangi.

Serikali ya Kenya inatumia app mpya ya simu kuwaelimisha wasichana kuhusu afya ya hedhi. Kupitia app ya Oky Kenya, watumiaji wanaweza kupata habari kuhusu usafi na masuala mengine.

Lengo ni kuzima hadithi na dhana potofu kuhusu hedhi na kuwalinda wasichana dhidi ya mimba za utotoni.

Katika kituo cha afya cha LVCT mjini Nairobi wafanyakazi wanajibu simu na ujumbe wa maandishi kutoka kote nchini. Wanasema maswali mengi yanahusu afya ya uzazi, hasa kuhuzu mzunguko wa hedhi.

Hedhi mara nyingi inagubikwa na usiri na aibu nchini Kenya, kwa mujibu wa UNICEF. Shirika hilo linasema wasichana vijana mara nyingi wanatafuta habari kwenye mitandao, lakini wanachokipata siyo sahihi.

Kuwasaidia, serikali ya Kenya, UNICEF na LVCT Health wamebuni Oky Kenya, app ya simu ambayo inawaruhusu wasichana wadogo kujifunza kuhusu miili yao kwa siri.

Akizungumza na Sauti ya Amerika, Kate Ogutu, Mshauri wa Afya alisema “Inawaambia kuwa kupata hedhi, hilo ni jambo la kawaida. Siyo kitu cha kuona aibu. Wanakuwa na uwezo wa kufahamu wapi wanaweza kupata bidhaa wanazohitaji. Pia inawasaidia kiakili, kwasababu baadhi ya watu hawafahamu kwanini wanapata hedhi. Wanashangaa, “kwanini napata damu?”

Cecilia Loku ni mmoja wa zaidi ya watu 8,000 ambao wanatumia app. Loku, mama wa mtoto mmoja, amesema ujauzito alioupata akiwa bado mdogo huenda angeweza kuuepuka kama angepata habari ambazo ziko kwenye app.

Muanzilishi wa shule ya sekondari ya Serene Haven Elizabeth Wanjiru takizungumza na Josephine Wanjiru mwenye umri wa miaka 19 akiwa na mtoto wake nje ya bweni
Muanzilishi wa shule ya sekondari ya Serene Haven Elizabeth Wanjiru takizungumza na Josephine Wanjiru mwenye umri wa miaka 19 akiwa na mtoto wake nje ya bweni

Mtumiaji huyo wa Oky Kenya App alieleza

“Kama ningekuwa na habari kama hizi za katika app ningeweza kubashiri kuhusu hedhi zangu, siku salama, lini naweza kushika uja uzito. Nisingepata mimba, nisingekuwa mama hivi sasa.”

Kwa mujibu wa taasisi kadhaa za huduma za afya duniani, kujizuia – kujiweka kando na aina zote za harakati za mapenzi – ndiyo njia muafaka kwa asilimia 100 ili kuepuka mimba. Aina mbali mbali za uzazi wa mpango, kama vile kutumia vidonge vya uzazi wa mpango au kondom, pia kwa kiasi kikubwa kunapunguza athari za kushikwa uja uzito.

Watumiaji wa Oky Kenya hawawezi tu kufuatilia mizunguko yao ya hedhi kwenye app lakini pia ujumbe wa maandishi au kuongea na washauri wao na kujifunza kuhusu haki ya afya ya uzazi.

Kate Kiama ni mkurugenzi wa mipango na matokeo katika She’s The First, taasisi yenye makao yake Marekani inayowasaidia wasichana ambayo inafanya kazi nchini Kenya na kusaidia katika app. Anasema uvumbuzi kama wa app unahitajika sana katika jamii ambayo inajiweka kando na kujadili afya ya mapenzi na uzazi.

“Washauri hasa wanajiweka kando kuzungumza na wasichana kuhusu kubalehe kwao, iwe ni kuhusu usafi wa hedhi. Unaweza kufikia msichana ambaye anakuja kutoka kwenye jamii ambaya anadhani hedhi ni mwiko, msichana huyu hana haja ya kumuelezea huu ni mchakato wa kawaida wa kibaiolojia.” alisema Kiama.

Wasichana wakienda shule huko Kibera
Wasichana wakienda shule huko Kibera

Kwa wastani wasichana wanne kati ya kumi nchini Kenya wana ujauzito au wana mtoto, kwa mujibu wa Wizara ya Afya.

Katika mahojiano kwa njia ya simu, naibu mkuu wa wizara, Janet Mule, amesema umaskini na ukosefu wa elimu, hasa katika maeneo ya mashambani, hali si nzuri.

Serikali ilizindua sera ya miaka 10 ya afya ya uzazi mwaka 2022 ambayo imeelezea hatua za kupunguza mimba za utotoni, kama vile kuhamasisha ufahamu kuhusu mzunguko wa hedhi na matumizi ya uzazi wa mpango.

Mamlaka nchini Kenya inaamini nyenzo kama app ya Oky Kenya itawasaidia wasichana kupata habari wanazohitaji.

Forum

XS
SM
MD
LG