Shambulio hilo lilitokea Jumatatu wakati waziri wa Uchukuzi alipokuwa akisafiri kwenye barabara kuu kusini mwa jiji la Johannesburg, polisi walisema.
"Matairi ya gari la Waziri yalitobolewa na misumari, na hivyo kusababisha gari kusimama na kuwawezesha wahalifu kuwapora watu waliokuwa ndani ya gari," ilisema taarifa ya wizara ya uchukuzi.
Waziri na walinzi wake walitoka katika janga hilo "bila kujeruhiwa na salama", iliongeza. Msemaji wa polisi Athlenda Mathe alisema majambazi hao walitoroka wakiwa na mali binafsi za watu waliokuwemo ndani ya gari hiyo na bastola mbili zanazomilikiwa na Jeshi la Polisi la Afrika Kusini (SAPS).
"Msako wa kuwatafuta waliohusika umeanzishwa kufuatia tukio hili lisilo la kawaida” Mathe alisema. Tukio hilo ambalo linamuhusisha afisa wa ngazi ya juu akiwa na walinzi waliokuwa na silaha, ni tukio la kushangaza hata kwa viwango vya Afrika Kusini.
Polisi wamerekodi matukio ya ujambazi zaidi ya 500 na takriban mauaji 70 kwa siku katika nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 62 kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu, kulingana na takwimu rasmi.
Forum