Licha ya mwanafunzi huyo kutoka mkoa wa Kigoma kupata ufadhili wa masomo wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) kutoka serikalini, anahitajika kupeleka katika idara ya uhamiaji cheti chake cha kuzaliwa, cha baba yake, mama yake, cha bibi na babu mzaa baba na mzaa mama.
Taarifa iliyotolewa na mwanasheria wa muungano wa wanafunzi Tanzania inaeleza kwamba Abdul Nondo, amefikishwa katika makao makuu ya ofisi za uhamiaji, na kutakiwa kuthibitisha uraia wake.
Kati ya vyeti anayotakiwa kuwasilisha kwa maafisa wa uhamiaji ni pamoja na cheti chake cha kuzaliwa, cheti cha kuzaliwa cha baba yake, mama yake, cha bibi na babu mzaa baba na mzaa mama, na vyeti vya ndugu zake ifikapo Aprili 20 bila kukosa.
Lakini mbunge wa Kigoma Mjini, anakotoka kijana huyo, Zitto Kabwe, anasema lazima atafuatilia kwa karibu uchunguzi huo.
“Yeye atatoa wapi cheti cha kuzaliwa cha babu yake? Hata huyu ambaye amemwagiza hivi vitu, hawezi kupata cheti ya babu yake mwenyewe. Sasa mazingira kama haya ni kutaka kumtisha ili kumfanya aache shughuli zake za harakati” amesema mbunge Zitto Kabwe katika mahojiano ya simu na sauti ya Amerika.
Maafisa wa uhamiaji wa mkoa wa Kigoma, wanasema kuwa sheria inawaruhusu kumhoji mtu yeyote wanaye mtilia mashaka uraia wake na kuwa wana mashaka na uraia wa Abdul Nondo, hivyo awathibitishie kuwa yeye ni Raia wa Tanzania. Lakini wakili wa kijana huyo, Reginald Martin, anasema hatua hiyo ina hila.
“Unaweza tu ukapata mwelekeo ya kwamba nia yao ni nini kwa sababu Abdul Nondo ni mwanafunzi wa chuo, ana vigezo vyote kwa sababu ni miongoni mwa wanafunzi wanoapata ufadhili wa masomo kutoka serikalini. Serikali haiwezi kumdhamini mtu au kumlipia karo, mtu ambaye sio raia wa Tanzania,” ameeleza wakili wa Abdul Nondo, Regmald Matin.
Uchunguzi wa uraia wa Abdul Nondo pia umezua hoja kwamba wakazi wa mkoa wa Kigoma, wanadhulumiwa na serikali. Mbunge Zitto Kabwe, amesema atafuatana na mwanafunzi huyo hadi katika ofisi za uhamiaji, akilalamika kwamba mara nyingi, raia wa Kigoma wanaendewa kinyume na serikali.
“Imekuwa ni tabia sasa kwamba wanapojitokeza wanasiasa na wananchi wenye kuhoji utenda kazi wa serikali, ikitokea tu kwamba anatoka Kigoma au mikoa ya pembezoni, wanachukuliwa kama sio raia wa Tanzania. Ndio maana nimesema kwamba nitampeleka huyu Kijana Abdul Nondo katika ofisi za uhamiaji, na watuambie kama watu wa Kigoma sio watanzania”
Mbunge huyo pia amewataka wakazi wa Kigoma kuandamana naye hadi ofisi za uhamiaji pindi atakapo msindikiza Abdul Nondo. Sauti ya Amerika ilipomuuliza kama hatua yake ya kutaka wakazi wa Kigoma kuandamana naye hadi katika ofisi za uhamiaji haitachukuliwa kama maandamano ambayo yamepigwa marufuku na serikali haitachukuliwa kama uvunjaji wa sharia, mbunge huyo amesema kwamba hatajali jinsi matamshi na vitendo vyake vitakavyotafsiriwa.
Abdul Nondo, mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam, anakabiliwa na mashtaka ya kutoa habari za uongo kwamba alitekwa nyara mnamo tarehe 6 mwezi machi mwaka huu, baada ya kutoweka katika mazingira tatanishi na baadae kuripoti polisi.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington, DC