Takriban waumini 30 wa kanisa wanaaminika wamekwama katika kifusi hicho wakati paa hilo lilipoporomoka, maafisa walisema. Waokoaji walikuwa wakitambaa chini ya nguzo za paa hilo na maafisa walileta mbwa kusaidia katika zoezi hilo kuwatafuta watakao kuwa wamenusurika.
Polisi ya jimbo la Tamaulipas walisema kuwa karibu watu 100 walikuwa kanisani wakati paa hilo lilipoporomoka.
Ofisi ya msemaji wa usalama wa jimbo hilo alisema jioni Jumapili kuwa watu tisa walikuwa wamethibitishwa kufariki kutokana na kuanguka kwa paa hilo, na kueleza kuwa kuna uwezekano mkubwa kulisababishwa na “udhaifu wa ujenzi.”
Polisi wa jimbo la Tamaulipas alisema vikosi vya Jeshi la Taifa, polisi wa jimbo na ofisi ya ulinzi wa raia ya jimbo na shirika la Msalaba Mwekundu walishiriki katika operesheni hiyo.
Baraza la Mexico la Maaskofu lilitoa taarifa likisema kuwa “tunaungana katika sala kwa janga hili la wale waliofariki na wale waliojeruhiwa.”
Mchungaji Jose Armando Alvarez wa Dayosisi ya Kanisa Katoliki ya Tampico alisema paa liliporomoka wakati waumini walipokuwa wanapokea communio katika kanisa la Santa Cruz katika mji wa Ghuba ya pwani ya Ciudad Madero, iliyoko jirani na mji wa bandari wa Tampico.
Dayosisi hiyo baadae ilibandika orodha ya watu takriban 50 ambao walikuwa wamelazwa hospitali kutokana na ajali hiyo. Walikuwemo mtoto wa miezi 4, watoto watatu wenye umri wa miaka mitano na wawili wenye umri wa miaka 9. Hapakuwa na taarifa ya mara moja kuhusu hali zao.
Idadi ya watoto waliofariki – maafisa wa polisi walisema watatu kati ya waliofariki ni watoto – inawezekana ilikuwa kwa sababu ubatizo ulikuwa ufanyike katika kanisa hilo.
“Tuna majonzi ya kupoteza watu ambao walikuwa pale kusherehekea ubatizo wa watoto wao,” Alvarez aliandika.
Wakati huo huo, kulikuwa na dalili za matumaini.
“Chini ya kifusi hicho, shukran kwa Divine Providence na kazi ya timu za waokoaji, watu wametolewa wakiwa hai!” Dayosisi ya Alvarez iliandika katika taarifa iliyobandikwa kwenye mitandao ya kijamii. “Tuendelee Kusali!”
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AP.
Forum