Kuwasili kwa Maduro kutafuatiwa na mikutano kati ya ujumbe wa Venezuela, akiwemo makamu rais wa nchi hiyo na waziri wa mafuta, na maafisa wa China akiwemo waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi, mjini Shanghai, mapema wiki hii, kulingana na wizara ya mambo ya nje ya China.
Makamu Rais wa Venezuela Delcy Rodriguez alisema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X Ijumaa kuwa serikali hizo mbili zilikuwa zinaimarisha uhusiano wa pande mbili, na kupanua “mkakati wa ushirikiano na kazi za pamoja kimataifa, kwa ajili ya amani na heshima chini ya misingi na malengo ya mkataba wa UN.”
Ziara hiyo iko sambamba na mkutano wa viongozi wa G20 huko New Delhi wikiendi hii, ambapo rais wa China Xi Jinping hatahudhuria.
Maduro mara ya mwisho alizuru China mwaka 2018, ambapo alikutana na Xi mjini Beijing.
Uwekezaji katika sekta ya nishati na ushirikiano huenda yakawa ndio lengo kuu la ziara hiyo. China ni mnunuaji mkubwa wa mafuta ghafi, wakati Venezuela inajulikana kuwa na akiba kubwa ya mafuta hayo.
Licha ya vikwazo vya Marekani kwa mafuta ya Venezuela, China ilinunua takriban mapipa 283 milioni, au tani za metriki 38.8 milioni, za mafuta ghafi kutoka katika nchi hiyo mwaka jana, kulingana na takwimu zilizotolewa na Kpler. Usafirishaji mwingi zaidi wa mafuta ya Venezuela unapitia nchi ya tatu kama vile Malaysia.
China iliripoti kutoagiza mafuta ghafi kutoka Venezuela katika takwimu rasmi za forodha mwaka jana au hadi sasa mwaka huu.
Kampuni ya kichina inayomilikiwa na serikali ya PetroChina ina asilimia 40 ya hisa katika mradi wa Sinovensa huko katika ukanda wa Orinoco sambamba na kampuni ya serikali ya mafuta ya Venezuela PDVSA. Kampuni hiyo ilisitisha kusafirisha mafuta ya Venezuela mwezi Agosti 2019 baada ya uongozi wa Trump kuzidisha vikwazo dhidi ya msafirishaji wa Amerika Kusini.
Venezuela pia ina deni kubwa la China kufuatia mkataba wa mkopo wa mafuta wa dola wa bilioni 50 uliofikiwa mwaka 2007 wakati huo rais Hugo Chavez akiwa madarakani.
Mwaka 2020, uongozi wa Maduro na mabenki ya China walikubaliana kipindi cha kutolipa deni hilo la takriban dola bilioni 19, kulingana na taarifa ya Reuters.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters.
Forum