Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 19:43

Mkuu wa Mawaziri Kenya asema serikali inahitaji miaka miwili kufufua uchumi


Mkuu wa Mawaziri Kenya, Musalia Mudavadi,
Mkuu wa Mawaziri Kenya, Musalia Mudavadi,

Serikali ya Kenya inasema inahitaji angalau miaka miwili kufufua uchumi wa nchi hiyo na Wakenya wanapaswa kujipanga kukabiliana na ugumu wa maisha.

Kauli hiyo inahusisha changamoto za sasa za gharama ya juu ya maisha na deni la umma na vita vya Russia nchini Ukraine."

Mkuu wa Mawaziri Kenya, Musalia Mudavadi, alisema bungeni Jumatano, kuwa serikali haina udhibiti wa sababu zinazochangia gharama ya juu ya maisha na nchi iko katika matatizo ya kiuchumi ya muda mrefu

Wakati wa kujibu maswali bungeni Jumatano, kuhusu jitihada za serikali kupunguza gharama za bidhaa za msingi, Musalia Mudavadi, waziri wa zamani wa fedha Kenya, ameeleza kwa sasa serikali ya Rais William Ruto inakumbana na vizingiti vingi vinavyotatiza jitihada zilizopo kukwamua na kuleta utulivu wa uchumi wa Kenya kwa kasi inayotarajiwa kwa raia wake.

Rais wa Kenya William Ruto
Rais wa Kenya William Ruto

Alisema serikali hiyo itahitaji muda wa miaka miwili kushusha chini gharama ya juu ya maisha.

Aidha, Bw Mudavadi, ameelezea kuwa katika mkakati wa muda mfupi wa kuwalinda raia wa Kenya dhidi ya hali mbaya ya uchumi, serikali imelazimika kuondoa ushuru wa bidhaa za chakula kutoka nje ya nchi, kupunguza uagizaji wa mazao kutoka nje na kupanda mazao yanayostahimili ukame, kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, kusaidia katika juhudi za kupunguza gharama za maisha na kusaidia kupunguza upungufu wa chakula na vile vile kurejesha chini gharama ya bidhaa za msingi.

Serikali ya Ruto imelazimika kuyaruhusu makampuni binafsi kuagiza tani milioni 1.5 za mahindi na mchele kutoka mataifa ya kigeni bila kulipiwa ushuru ili kukabiliana na baa la njaa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 40, kuiwezesha nchi kuwa na hifadhi ya kutosha hadi mavuno yajayo kuanzia Julai-Agosti mwaka huu.

Ruto amekuwa akieleza kuwa serikali yake ina mkakati thabiti wa kufufua uchumi wa Kenya lakini kufanya hivyo kunategemea msimu wa mvua nyingi ukiambatana na mkakati wa serikali yake wa kuvuna maji kupitia mabwawa wala si kutegemea ruzuku aliyoiondoa iliyokuwa imewekwa kwenye unga wa mahindi, mafuta, na umeme na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta.

Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta

Hata hivyo, serikali yake huenda ikajikuta tena kwenye shinikizo la upinzani ambao umetangaza duru mpya ya maandamano ya kila wiki dhidi ya serikali yake kuanzia mwezi wa Mei tarehe 2 kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha na haki katika uchaguzi.

Aidha, mtaalamu wa uchumi Bw Charles Karisa anaeleza kuwa utendakazi wa serikali huenda ukavurugika kwa kiasi kikubwa iwapo maandamano ya upinzani yataendelea.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika, Nairobi

XS
SM
MD
LG