Boti hiyo ilikuwa imebeba watalii 31 kutoka nchi tofauti ikiwa pia na wafanyakazi 13, mamlaka ya jimbo la bahari ya Shamu imesema. Watu 16 hawajulikani walipo, 12 wakiwa raia wa kigeni na wanne wakiwa raia wa Misri.
Ripoti zinasema kuwa boti hiyo inamilikiwa na raia wa Misri. Miongoni mwa watalii waliokuwa ndani ni kutoka Ubelgiji, Uingereza, China, Finland, Ujerumani, Ireland, Poland, Slovakia, Uhispania, Uswizi na Marekani.
Boti hiyo ilianza safari yake Jumapili ikitokea kwenye bandari ya Ghalib karibu na mji wa Marsa Alam kusini mashariki mwa Misri, na ilikuwa itie nanga Ijumaa kwenye mji wa Hurghada uliopo kilomita 200 kaskazini mwa Misri.
Gavana wa eneo la tukio Amr Hanafi amesema kuwa baadhi ya manusura waliokolewa kwa ndege, huku wengine wakiokolewa kwa kutumia meli ya kivita.