Zaidi ya wahamiaji 10,000 wamefariki mwaka 2024 wakijaribu kufika Uhispania

Wahamiaji wakipanda boti ya usafirishaji haramu wakijaribu kuvuka njia ya bahari huko Saint Etienne Ufaransa, Oktoba 30, 2024. Picha ya AFP

Wahamiaji zaidi ya 10,000 walifariki dunia au kupotea mwaka 2024 wakati wakijaribu kufika Uhispania kwa njia ya bahari, shirika lisilo la kiserikali limesema Alhamisi, idadi hiyo ikiwa imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka uliopita na kubwa zaidi tangu mwaka 2007.

Ongezeko hilo la asilimia 58 linajumuisha watoto 1,538 na wanawake 421, kundi la kutetea haki za wahamiaji Caminando Fronteras limesema katika ripoti yake ambayo imeangazia matukio ya kipindi cha tangu Januari 1 hadi Disemba 5, 2024.

Shirika hilo limehesabu wastani wa wahamiaji 30 waliofariki kwa siku, zaidi ya wastani wa vifo18 kwa siku mwaka 2023.

Kundi hilo limekusanya takwimu zake kutokana na simu za dharura walizowekewa wahamiaji kwenye meli zilizo katika shida ili kuomba msaada, familia za wahamiaji waliotoweka na takwimu rasmi kutoka idara za uokoaji.

Limesema idadi ya vifo iliongezeka kutokana na kutumia boti chakavu na njia hatari pamoja na uwezo duni wa huduma za uokoaji baharini.