Mazishi hayo yameongozwa na waziri mkuu wa nchi hiyo Dk. Edouard Ngirente katika mji wa Rubavu ulioko magharibi mwa Rwanda. Waziri Mkuu alisema kwamba huenda idadi ya vifo ikaongezeka kwa kuwa baadhi ya miili inaendelea kutafutwa.
“Kuna idadi ya watu ambao tunaendelea kuwatafuta na huenda idadi ya waathirika ikaongezeka, kusema ukweli hili ni janga lililoiangukia nchi yetu, kufuatia maji mengi ya mvua, yaliyomomonyoa udongo na kusababisha nyumba kuwaangukia watu, tunatambua uchungu na matatizo mnayoyapitia” alisema waziri mkuu Ngirente na kuongezea, “sisi kama serikali tutajitahidi kuwapa msaada kadri iwezekanavyo ndiyo mimi mwenyewe niko hapa nikimwakilisha rais ambaye kuanzia jana amekuwa akiwapa taarifa kuhusu msimamo wa serikali.”
Simanzi na machozi vilitawala katika maeneo hayo, baada ya mvua kubwa kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Baadhi ya watu waliopoteza familia zao walilielezea tukio hilo wakati wakizungumza na Sauti ya Amerika na kuelezea kuwa waathirika walifunikwa na vifusi vya nyumba na kingo za mlima.
“Kifusi kilianguka na kutufunika mimi na mume wangu na mtoto wetu, nilipozinduka nikaona mimi kichwa changu bado kinaonekana na mume wangu akaanza kunivuta, lakini tulipoangalia vizuri alipokuwa amelala mtoto wetu, tukakuta yeye kimemfunika kabisa, tukajaribu kuondoa matofali lakini tulishindwa na tuliposhindwa ndiyo nikapanda ukuta na kutoka nje kwenda kuomba msaada,” alisema raia mmoja.
Muathirika mwingine alikuwa ni Gashonga Jean Marie Vianney, ambaye amewapoteza watoto wake watatu wa kike kwa mpigo.
“Kifusi cha mlima kilimegeka na kuangukia nyumba yetu upande wa juu karibu na chumba cha watoto wangu wa kike na wa kiume, na mara moja kikafunika chumba cha watoto wangu watatu wa kike waliokuwa pamoja na kufariki papo hapo, upande wa chumba cha wavulana wao waliweza kujivuta na kutoka na ndiyo wamemsaidia mama yao na kumuondoa kwenye vifusi vingine.”
Mpaka sasa serikali imepeleka msaada wa tani 60 za vyakula mbalimbali kwa waathirika ambao wengi wao wamepewa hifadhi kwenye majengo ya shule, makanisa huku baadhi yao kupewa hifadhi na jamaa na maarafiki.
Hata hivyo kampeni imeanza kuzihamisha zaidi ya familia 137 kutoka maeneo hatarishi na kuwataka watu wanaoishi katika maeneo jirani na kingo za milima mirefu kuyahama maeneo hayo.
Waziri anayehusika na majanga nchini Rwanda Marie Solange Kayisire alisema, “Tunawataka watu kuwa makini, hasa wale wenye kuishi karibu na kingo za milima mirefu kuyahama maeneo hayo haraka ili wasije kuangukiwa na kingo hizo za milima.”
Na kuongeza kuwa “Ili tusiendelee kupoteza maisha ya watu, mali zinaweza kupotea ndiyo lakini linapokuja suala la maisha ya watu wakiwemo watoto wadogo inakuwa ni hatari zaidi.”
Wakati serikali imewatahadharisha watu wanaoishi katika maeneo jirani na kingo za milima mirefu na kuwataka kuyahama maeneo hayo haraka ili kuepuka kuangukiwa na kingo hizo za milima.
Mwaka 2020 zaidi ya watu 80 walipoteza maisha kufuatia mvua kubwa, tangu wakati huo kumekuwepo na juhudi za kuwahamisha watu walioko katika maeneo hatarishi, na kuwajengea makazi mengine. Hii ni mara ya kwanza kupoteza idadi kubwa ya watu kwa usiku mmoja.
Salamu za rambirambi zimeendelea kutolewa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kimataifa akiwemo mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika Musa Faki Mahamat.
IMETAYARISHWA NA SYLIVANUS KAREMERA, VOA, KIGALI.