Maafisa hao wataripoti katika vituo vyao vipya vya kazi kuanzia Juni 15, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa, Monica Juma.
Katika barua iliyotolewa na wizara, Juma amesema maafisa hao watatumikia nafasi hizo kwa kipindi cha miaka minne, gazeti la Daily Nation limeripoti.
Hatua hiyo imekuja wakati serikali inapambana na kashfa ya rushwa inayohusisha taasisi za serikali.
Mwaka 2016, Mkaguzi Mkuu wa serikali aliripoti kuwa balozi kadhaa hazikuweza kuonyesha jinsi stika za visa na pasi za kusafiria zenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 zilivyotumika, ikionyesha udhaifu uliokuwepo katika kutunza rikodi katika balozi hizo na kutia wasiwasi juu ya kuwepo vitendo vya wizi.
Ripoti hiyo imesema kuwa Idara ya Uhamiaji iliweza kuonyesha matumizi ya pasi za kusafiria na stika za visa zenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 tu ukilinganisha na nyaraka kama hizo za thamani ya bilioni 2.9 zilizokabidhiwa katika balozi hizo.
Juma amesema kuwa maafisa hao watapewa mafunzo na kupitishwa na Chuo cha Mafunzo ya Diplomasia (FSA) baada ya kufanyiwa mtihani na kufaulu kabla ya kuanza kazi.