Ruto, ambaye alihudumu kama naibu wa rais wa Kenya kwa miaka 10, anachukua hatamu za uongozi wakati wa bei za vyakula na mafuta ziko juu, ukosefu mkubwa wa ajira na kuongezeka kwa deni la umma.
Kufikia saa kumi na moja alfajiri uwanja wa michezo wa Kasarani jijini Nairobi wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000 ulikuwa umejaa wafuasi wa Ruto waliovalia rangi za njano na kijani za chama chake. Walicheza na kupeperusha bendera ndogo za kitaifa wakifuatilia miziki ya bendi.
"Ni kijana mwenzetu! Najua atatuletea fursa zaidi," alisema dansa Juma Dominic huku yeye na kundi lake wakijiandaa,.
Idara ya taifa ya Polisi ilikuwa imeandika kwenye Twitter kwamba uwanja huo ulikuwa umejaa saa 11 alfajiri na kuwataka raia kukaa nyumbani, lakini umati wa watu uliendelea kujaribu kuingia kwa nguvu. Huduma ya Ambulance ya St John ilisema imewapeleka watu kadhaa waliojeruhiwa hospitali.