WHO yaanza kukabiliana na mlipuko mpya wa Ebola Afrika Magharibi

Matshidiso Moeti

Shirika la Afya Duniani, WHO, limeeleza wasiwasi wake kutokana na kuibuka tena kwa ugonjwa wa Ebola huko Afrika Magharibi na kuanzisha mara moja juhudi za kukabiliana na mlipuko huo.

Wizara ya Afya ya Guinea ilitangaza mlipuko huo Jumapili miaka mitano baada ya taifa hilo kutangaza kwamba hakuna tena Ebola nchini humo.

Maafisa wa afya walitangaza janga jipya Jumapili kufuatia vifo vya watu watatu na wanne kuambukizwa kuanzia mapema mwezi Februari.

Maafisa wa Afya wameweza kufuatilia na kugundua mlipuko ulianza Februari 1, wakati watu walipokwenda kumzika muuguzi kutoka kituo cha afya cha wilaya.

Mkurugenzi wa WHO, kanda ya Afrika, Matshidiso Moeti amesema shirika lake linajitayarisha kwa haraka kuweza kukabiliana na hali hiyo.

Rais wa Liberia George Weah amewaamrisha wakuu wa afya kuimarisha uchunguzi na kufuatilia uwezekano wa kuzuka mlipuko nchini humo.