WHO inasema ugonjwa unaoshukiwa kuwa Marburg umeua watu wanane Tanzania

Mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Gebreyesus akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Kigali kuhusu mlipuko wa Marburg, Oktoba 20, 2024. Picha ya Reuters

Shirika la afya duniani WHO Jumanne limesema kwamba mlipuko unaoshukiwa wa ugonjwa hatari wa Marburg nchini Tanzania umewaua watu wanane, na kuonya kwamba hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo nchini humo ni “kubwa”.

Idara hiyo ya afya ya Umoja wa Mataifa imesema ilitoa taarifa kwa nchi wanachama siku ya Jumatatu kuhusu “mlipuko unaoshukiwa wa ugonjwa wa virusi vya Marburg katika mkoa wa Tanzania wa Kagera”.

“Tunayo taarifa ya kesi tisa kufikia sasa, ikiwa ni pamoja na watu wanane ambao wamefariki. Tunatarajia kesi zaidi katika siku zijazo kadri uchunguzi wa ugonjwa unavyoendelea,” mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema kwenye mtandao wa X.

Ameongeza kuwa “WHO imetoa msaada wake kamili kwa serikali ya Tanzania na kwa jamii zilizoathirika.”

Tangazo hilo linajiri chini ya zaidi ya mwezi mmoja baada ya WHO kutangaza kuwa mlipuko wa Marburg katika nchi Jirani ya Rwanda ambao uliua watu 15 umedhibitiwa kabisa.

Marburg husababisha homa ya kutokwa na damu inayoambukiza sana. Virusi hivyo vinaambukizwa kutoka kwa popo na ni vya familia moja kama virusi vya Ebola.