Watu wasiopungua wanne wafariki katika ajali ya jengo Florida

Kikundi cha uokoaji kinaendelea kutafuta wakazi wa jengo ambalo liliporomoka upande mmoja, karibu na Pwani ya Miami, Florida, Marekani., June 24, 2021.

Idadi ya watu waliopoteza maisha yao kutokana na kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika Kaunti ya Miami Dade, jimbo la Florida, hapa Marekani, imeongezeka na kufikia hadi angalau wanne.

Hadi tukitayarisha ripoti hii, zaidi ya watu 150, walikuwa hawajulikani waliko, huku waokoaji wakiendelea kuwatafuta manusura kwenye vifusi.

Rais wa Marekani Joe Biden, aliridhia tangazo la hali ya dharura, katika jimbo la Florida, na akaamuru kwamba, msaada utolewe na serikali kuu, ili kusaidia juhudi za uokozi, za maafisa wa jimbo na kaunti hiyo.

Hatua hiyo ya rais, inalipatia idhini shirika la kitaifa la majanga, Fema, kuratibu na kuongoza juhudi zote, za uokozi, White House imesema Ijumaa.

Hata hivyo, kilichosababisha kuporomoka kwa jengo hilo, ambalo lilijengwa miaka arobaini iliyopita, bado hakijajulikana, ingawa maafisa walisema, lilikuwa likifanyiwa ukarabati kwenye paa lake.

Vyanzo vya Habari : AP/ Reuters