Watu tisa wafariki nchini Chad katika milipuko kwenye ghala la zana za kijeshi

Ramani ya Chad

Watu tisa walifariki na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa wakati moto uliposababisha milipuko katika ghala la zana za kijeshi katika mji mkuu wa Chad, afisa mmoja alisema Jumatano.

Msemaji wa serikali Abderaman Koulamallah alisema watu 46 walikuwa wakitibiwa majeraha mbalimbali baada ya milipuko hiyo kuwashtua wakazi kutoka usingizini Jumanne jioni katika wilaya ya Goudji katika mji mkuu, N’Djamena.

Koulamallah alisema hali kwa sasa imedhibitiwa.

Chanzo cha moto huo hakikufahamika mara moja, na Rais Mahamat Deby Itno alisema uchunguzi utafanyika.

“Amani kwa nafsi za waathirika, rambirambi za dhati kwa familia zilizofiwa na ahueni ya haraka kwa waliojeruhiwa,” Deby alisema kwenye ukurasa wa Facebook. Baadaye alitembelea eneo la ajali pamoja na hospitali ambako majeruhi walikuwa wakitibiwa.