Watu 48 wapatikana wamefariki wakiwa kwenye lori Marekani

Waombolezaji wakusanyika katika eneo ambapo watu wasiopungua 46 walipatikana wakiwa wamefariki.

Watu 46 wamepatikana wamefariki wakiwa kwenye trela ya trekta katika barabara moja mjini San Antonio, jimbo la Texas, Marekani.

Huo ndio mkasa wa hivi karibuni kabisa, uliopelekea vifo vya wahamiaji waliokuwa wakisafirishwa, wakivuka mpaka kutoka Mexico hadi Marekani.

Watu kumi na sita walilazwa hospitalini, wakiwemo watoto wanne. Mfanyakazi mmoja wa jiji alisikia kilio cha kuomba msaada kutoka kwa lori muda mfupi kabla ya saa kumi na mbili jioni, jana Jumatatu, na kugundua tukio hilo la kutisha, Mkuu wa Polisi William McManus alisema.

Saa kadhaa baadaye, mifuko ya miili ilikuwa imetandazwa chini, karibu na trela, ikionyesha taswira ya kusikitisha ya msiba huo.

Meya wa San Antonio Ron Nirenberg aliuita mkasa huo, “janga la kibinadamu” na kusema watu 46 waliokufa walikuwa na "familia ambazo labda zilikuwa zikijaribu kutafuta maisha bora."

Ni miongoni mwa mikasa mibaya zaidi kuwahi katika miongo ya hivi karibuni. Mnamo mwaka wa 2017, Wahamiaji kumi walipatikana wakiwa wamekufa baada ya kunaswa ndani ya lori lililokuwa limeegeshwa kwenye duka la Walmart mjini San Antonio.

Mnamo mwaka wa 2003, wahamiaji 19 walipatikana katika lori lililokuwa na joto kupita kiasi kusini mashariki mwa San Antonio.