Watu 341 wamefariki kutokana na marufiko nchini Chad

Nyumba zilizojaa maji baada ya mafuriko makubwa mjini N'djamena, Chad, Oktoba 14, 2022. Picha ya Reuters

Mafuriko makubwa ya wiki kadhaa nchini Chad yamesababisha vifo vya watu 341 na wengine milioni 1.5 wameathirika tangu mwezi Julai, Umoja wa Mataifa ulisema Jumatatu.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu (OCHA) ilisema majimbo 23 ya nchi hiyo yalikumbwa na mafuriko hayo.

Ilitaja takwimu za serikali ambazo zilisema baadhi ya nyumba 164,000 zimeharibiwa, na karibu ng’ombe 70,000 walikufa na ekari 640,000 za mashamba ziliharibiwa pia.

Serikali bado haijatangaza takwimu rasmi za uharibifu huo uliosababishwa na mafuriko ambayo yamekumba taifa hilo lenye watu milioni 16.

Wiki iliyopita, wanafunzi 14 na mwalimu wao walifariki wakati basi lao lilipoanguka baada ya mvua kubwa kunyesha katika jimbo la Ouaddai katika eneo la mashariki lenye ukame.

Kufikia katikati mwa mwezi Agosti, watu 54 walipoteza maisha katika mafuriko katika jimbo la Tibesti, katika jangwa la Chad eneo la mbali la kaskazini.