Polisi nchini Nigeria Jumapili wamesema idadi ya vifo katika matukio mawili ya mkanyagano nje ya vituo vya kugawa chakula kwa watu maskini imeongezeka hadi 32.
Watu 22 walifariki Jumamosi wakati walipokuwa kwenye foleni nje ya kituo cha kugawa mchele katika mji wa kusini wa Okija, polisi wamesema, baada ya taarifa ya kushtusha ya awali kwamba “wengi” walifariki katika tukio hilo.
Na siku hiyo hiyo mkanyagano tofauti nje ya kanisa lililokuwa linagawa chakula kwa “watu wanaoishi katika mazingira hatarishi na wazee” katika mji mkuu Abuja uliua watu 10, na kumfanya Rais wa Nigeria Bola Tinubu kubadili ratiba yake kutokana na misiba hiyo miwili.
Mikanyagano hiyo nje ya vituo vya kugawa chakula inatokea huku taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika likikabiliwa na mzozo mbaya wa kiuchumi katika miaka ya hivi karibuni, mfumuko wa bei ukiongezeka kwa asilimia 34.6 mwezi Novemba.