Watu 19 wauawa katika mapigano kwenye Ikulu ya Chad

Rais wa Chad Jenerali Mahamat Idriss Deby Itno

Watu wenye silaha Jumatano waliishambulia Ikulu ya Chad katika mji mkuu N’Djamena, na kuzua mapigano ambayo yaliua washambuliaji 18 na afisa mmoja wa usalama na wengine kadhaa kujeruhiwa, serikali ilisema.

Waandishi wa habari wa AFP walisikia milio ya risasi karibu na Ikulu mjini N’Djamena, huku vifaru vikionekana barabarani, vyanzo vya usalama vimeripoti kuwa watu wenye silaha walijaribu kuvamia jengo hilo.

Serikali baadaye ilisema watu 19 waliuawa katika mapigano hayo, 18 kati yao walikuwa washambuliaji wa kundi la watu 24 ambalo lilifanya shambulizi hilo.

“Kuna watu 18 waliofariki na sita kujeruhiwa” miongoni mwa washambuliaji” tulipata kifo kimoja na watatu waliojeruhiwa na mmoja kati yao alijeruhiwa vibaya”, msemaji wa serikali na waziri wa mambo ya nje Abderaman Koulamallah aliiambia AFP.

Saa chache baada ya shambulizi hilo, Koulamallah alionekana kwenye video kwenye mtandao wa Facebook, akiwa amezungukwa na wanajeshi, akisema kwamba “hali imedhibitiwa kabisa, jaribio la kuvuruga usalama limezimwa.”

Vyanzo kadhaa vya usalama vilisema kwamba kundi la washambuliaji wenye silaha walifyatua risasi ndani ya ofisi ya rais Jumatano jioni, saa moja na dakika 45 majira ya huko, kabla ya kuzidiwa nguvu na walinzi wa rais.

Barabara zote zinazoelekea kwenye ofisi ya rais zilifungwa na vifaru vilionekana barabarani, kulingana na mwandishi wa AFP aliyekuwa kwenye eneo la tukio.