Washukiwa wa ugaidi waachiliwa huru Kenya

Washukiwa wa ugaidi nchini Kenya wakiwa mahakamani kabla ya kuachiwa huru.

Vijana 17 kati yao wanawake wawili waliokuwa wanashukiwa kujihusisha na kundi la kigaidi la Al-Shabab wameachiliwa huru Jumatatu na mahakama ya Kwale nchini Kenya.

Vijana hao wenye umri wa miaka 18 hadi 28 walikamatwa January 28, 2019 na kufikishwa mahakamani na maafisa wa polisi waliomba mahakama iwape muda wa kufanya uchunguzi zaidi.

Akitoa uamuzi huo , hakimu wa mahakama ya Kwale Dominica Nyambu , polisi hawakutoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha juu ya kujihusisha kwa vijana hao na ugaidi.

“Mkurugenzi wa umma hajaweza kutoa ushahidi wa kutosha na kwamba washukiwa wote wanaachiliwa na faili yao imefungwa," amesema hakimu Nyambu akitoa uamuzi.

Wakili wa washukiwa hao Raphael Chimera amepongeza uamuzi wa mahakama akisema upande wa mashtaka haukuwa na ushahidi wa kuwahusisha vijana hao na tuhuma za ugaidi.

Tangu shambulizi la kigaidi la Dusit kutokea jijini Nairobi ambapo watu 21 waliuawa na wengine kujeruhiwa , serikali ya Kenya imekuwa ikifanya msako wa kuwakamata washukiwa wa kundi la kigaidi la Al-Shabab.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Amina Chombo, Kenya.