Mawakili wamesema watu hao 10, wakiwemo wakuu wa vyama vya siasa na makundi ambayo yalisaini tangazo la mwezi Machi wakiomba kurejea kwa demokrasia, wanashutumiwa kwa kufanya mikutano haramu na kupanga njama dhidi ya “mamlaka halali”.
Waliofungwa jela ni miongoni mwa watu 11 waliokamatwa na kuwekwa kizuizini wiki iliyopita wakati wakifanya mkutano wa faragha katika mji mkuu wa Bamako, baada ya kuomba kurejeshwa kwa utawala wa kiraia. Serikali ya kijeshi ilipiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa.
Mmoja kati yao, waziri wa zamani wa sheria Mohamed Ali Bathily, aliachiwa huru Jumamosi iliyopita.
Jaji aliamua kwamba waliofungwa “walidhoofisha usalama na kupanga njama dhidi ya mamlaka halali, kukiuka amri ya rais kwa kufanya mkutano usio halali”, mmoja wa mawakili wao, Hyacinthe Kone aliiambia AFP.
“Sijaona makosa haya katika sheria yetu ya jinai. Badala yake serikali ndiyo ambayo siyo halali,” alisema Kone.
Upinzani umelaani hatua hiyo na kuitaja kuwa “ukiukwaji mwingine wa haki msingi za uhuru,” unaofanywa na utawala wa kijeshi.
Viongozi wa kijeshi ambao walichukua madaraka mwaka 2020, waliahidi kuandaa uchaguzi na kukabidhi madaraka kwa raia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, lakini baadaye waliahirisha uchaguzi huo kwa muda usiojulikana.