Maandamano hayo ni sehemu ya shinikizo la wafuasi wa mbunge Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine wakitaka aachiliwe huru. Pia waandamanaji kadhaa wamekamatwa na wanajeshi hao.
Wafuasi wa Bob Wine
Wafuasi wa Bobi Wine, walisikika wakiimba “nguvu za watu, nguvu zetu” waliwasha moto katikati ya barabara na kuzuiya magari yasipite na kusimamisha shughuli za kibiashara katika soko la Kiseka, barabara za Namirembe na Kikuubo, kabla ya kusambaa hadi katika mitaa ya Wandegeya, Makindye na Gayaza, yenye shughuli nyingi Zaidi jijini Kampala.
Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA anaripoti kuwa maandamano pia yameshuhudiwa katika miji ya Mityana na mkono. Siku ya jumapili, kifo cha mtu mmoja kiliripotiwa mjini Miyana baada ya kupigwa na risasi, polisi walipokuwa wakiwatawanya waandamanaji.
Maandamano Kenya
Maandamano pia yameripotiwa mjini Busia nchini Kenya, vijana wa Kenya wakitatiza usafiri wa mizigo na mafuta kuingia Uganda wakitaka Bobi Wine aachiliwe huru.
Kyagulanyi, ambaye pia ni mwanamziki mashuhuri, anazuiliwa katika kambi ya wanajeshi ya Makindye jiji Kampala, baada ya kukamatwa siku ya jumatatu wiki jana.
Madai ya Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amedai kwamba mbunge Bobi wine na wenzake, walikuwa wamelenga kumuua kwa kumpiga mawe, akigeukia vyombo vya habari akivishitumu kwa kile alichokitaja kama kueneza habari za uongo kwamba wanasaisa wa upinzani walipigwa na kuumia vibaya mikononi mwa maafisa wa polisi walipokuwa wakikamatwa.
“ukitupa mawe kwa mtu aliye karibu nawe, lengo ni kumuua” ameandika Museveni.
kupitia ukurasa wake wa Facebook, Museveni amekasirishwa na wanaosema taarifa iliyotolewa na ikulu ya rais kwamba gari lake lilipigwa mawe ni za uongo, akisisitiza kwamba Bobi Wine na wabunge wenzake 6, watajibu mashtaka ya kujaribu kuipindua serikali na kujaribu kumuua.
Wanaharakati wapaza sauti
Licha ya wanaharakati wa kuteteta haki za kibinadamu, mawakili na familia ya mbunge Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, kueleza vyombo vya habari kwamba mwanasiasa huyo yumo katika hali mbaya ya kiafya baada ya kupigwa vibaya na walinzi wake museveni SFC, Museveni anasema kwamba Bobi Wine, anayezuiliwa katika kambi ya jeshi ya Makindye jiji Kampala, hana tataizo lolote la afya.
“Nimeamua kuwauliza madaktari wa jeshi kwa sababu wana uwezo wa kushughulikia tatizo lolote la kiafya. Bobi Wine ametibiwa na madaktari akiwa Arua, Gulu, na Kampala. Hana matatizo yoyote” ameandika Museveni kwenye ukurasa wake wa facebook.
Museveni akanusha
lakini katika kile kinachoonekana kama kujikanganya, Museveni katika taarifa yake anasema kwamba mwanasiasa huyo amepokea matibabu ya kutosha, akiwa wilayani Arua baada ya kukamatwa, wilayani Gulu kabla ya kufikishwa katika mahakama ya kijeshi, na katika hospitali ya kijeshi ya Makindye, Kampala,
Maafisa wote waliomtembelea Bobi Wine kizuizini, akiwemo mkewe, ndugu yake, mawakili Asuman Basalirwa na Erias Lukwago, wanasema kwamba hali ya afya ya Bobi Wine si nzuri, na kwamba anahitaji matibabu ya dharura na kwamba hawezi kuzungumza, kuketi wala kusimama bila kusaidiwa. hakuna daktari kutoka nje ya kambi wala waandishi wa habari wamekubaliwa kumfikia.
Museveni pia anadai kwamba mbunge Francis Zaake, anayetibiwa katika hospitali Rubaga jijini Kampala alikopelekwa na maafisa wa jeshi baada ya kupigwa, amehepa kukamatwa na kwamba anatafutwa na maafisa wa polisi. Zaake amekuwa akipumua kwa uwezo wa mashine katika hospitalini.
Vijana wamjibu Museveni
Vijana nchini Uganda hata hivyo wamemjibu Museveni kupitia kwenye mitandao ya kijamii, wengi wao wakimtaka akome kuwaita wajukuu wake na kukema kitendo cha kumzuilia Bobi Wine, wakimtaka aachilie mwanamziki huyo bila masharti.
Ufalme wa Bunganda umtoa taarifa fupi ukionya kwamba matumizi ya nguvu na fujo kumaliza tofauti za kisiasa ni kichocheo cha machafuko zaidi, na kutaka serikali kuwapa fursa wabunge wote wanaozuiliwa kupata matibabu. ufalme wa Buganda umejitaja kama mtetezi wa katiba, ikiwa mara ya kwanza kwa ufalme huo wenye idadi kubwa ya wafuasi kuzungumzia maswala ya kisiasa moja kwa moja.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, VOA, Washington DC