Wanahabari waungana kususia Habari za Makonda

Paul Makonda

Waandishi wa habari Tanzania wametangaza kuacha kuandika ama kutangaza habari zinazomhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuanzia Jumatano mpaka itakavyoamuliwa vinginevyo.

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa kushirikiana na klabu ya waandishi wa habari Dar es salaam, DCPC na klabu za waandishi wa habari Tanzania, UTPC vimetangaza maamuzi hayo.

Akiongea na idhaa ya Kiswahili VOA Katibu Mkuu wa TEF , Neville Meena amesema utekelezaji wa agizo hili unaanza mara moja kwa vyombo vyote vya habari nchini, na utaendelea hadi pale itakapotangazwa au kuamriwa vinginevyo.

Klabu hizo mbili na TEF katika tamko lao kwa vyombo vya habari zimesema zinalaani vikali vitendo vya Mkuu wa Mkoa katika kuvamia chombo cha habari cha Clouds Media akiwa ameambatana na askari wenye silaha.

Pia vimelaani kitendo cha kutoa amri ya kulazimisha kurushwa hewani kwa kipindi cha televisheni, ikiwa pamoja na kupora kipindi, mali ya kituo cha clouds TV, kitendo ambacho ni mwendelezo wa matendo yake ya kutoa lugha za kejeli na matusi kwa waandishi wa habari ambao wamekuwa wakishiriki katika kazi mbalimbali mkoani Dar es Salaam.