Wanafunzi hao ni wa Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Lucky Vincent ya jijini Arusha.
Vyanzo vya habari vimesema Mwinjilisti maarufu duniani kutoka Shirika la Samaritan Purse, Bill Graham wa Marekani na ndiye atakaye gharamia kukodisha ndege maalumu aina ya DC 8 kupeleka wanafunzi waliojeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea wilayani Karatu, Arusha.
Watoto hao wameumia shingo, miguu na sehemu mbalimbali za miili yao. Kwa mujibu wa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyarandu aliyezungumza jana na waandishi wa habari mjini Arusha, gharama za kukodisha ndege kwenda Marekani si chini ya dola za Kimarekani 350,000 (Sh milioni 700).
Katika ajali hiyo watu 35 walipoteza maisha wakiwemo wanafunzi wa darasa la saba, walimu na dereva wa gari la shule ya msingi iitwayo Lucky Vincent ya Arusha. Basi hilo lilikuwa limebeba waalimuna dereva, msaidizi wake na wanafunzi 27. Ajali hiyo ilitokea baada ya basi la shule kutumbukia katika korongo refu la mto Marera wilayani Karatu.
Mbunge huyo ameongeza kusema kuwa gharama hizo ni nje ya matibabu, chakula na malazi kwa wakati wote ambao wagonjwa hao na wasindikizaji watakuwa nchini humo.
“Tumefanikiwa kupata ndege aina ya DC 8 kutoka Shirika la Samaritan Purse linaloongozwa na mtoto wa Billy Graham aitwaye Franklin kwa ajili ya kuwasafirisha watoto Doreen Mshana, Sadia Awadh na Wilson Tarimo na wazazi wao watatu, yaani mama zao,” alisema Nyarandu akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Aidha amesema watoto hao wataambatana na daktari wa hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Elias Mashalla na muuguzi Simphorosa Silalye. Kwa mujibu wa Nyalandu, ndege hiyo inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro KIA) leo jioni ikitokea Charlotte ,Jimbo la North Carolina, Marekani.