Wamiliki wa mabasi Tanzania watangaza mgomo nchi nzima

Ramani ya Tanzania

Chama cha wamiliki wa Mabasi (TABOA) na wamiliki wa malori na Chama cha wasafirishaji kimetangaza kwa pamoja mgomo wa usafirishaji abiria na mizigo nchi nzima.

Uamuzi huo umefanyika kwa ushirikiano wa vyama vyote vitatu Dar es Salaam kuanzia siku ya jumatatu ili kushinikiza serikali kutopitisha sheria ya usafirishaji inayotarajiwa kusomwa mara ya tatu na kupitishwa siku ya Jumanne wiki ijayo.

Akitoa maazimio hayo yaliofikiwa katika mkutano mkuu maalumu wa chama cha wamiliki wa mabasi, malori, daladala na bajaji, katibu mkuu wa TABOA Eneo Mrutu amesema sheria inayolenga kupitishwa haikuwashirikisha wadau na haitenganishi makosa ya dereva na mmiliki, hali inayosababisha kosa lililofanywa na dereva kusababisha mmiliki kufungwa jela.

Aidha amewaomba wabunge bila kujali itikadi za vyama vyao kutopisha sheria hiyo mpaka ifanyiwe marekebisho kwa kuwa inalenga kuharibu sekta ya usafirishaji nchini.

"Kinachosababisha mgomo wa wamiliki ni majukumu mapya kwa wasafirishaji chini ya kanuni mpya za Sumatra," baadhi ya wadau wameeleza hilo.

Wamesema kuwa majukumu haya yanapatikana katika rasimu ya Kanuni mpya za Usafirishaji Abiria Kifungu cha 21: Wajibu wa mmiliki/mwenye leseni na mtoa huduma.