20 wameuawa katika shambulizi mjini Rafah, hospitali ya Matyrs yasema

  • VOA News

Moshi unatoka eneo la mashambulizi yaliyofanywa na wanajeshi wa Israeli mjini Rafah, Ukanda wa Gaza. Mei 19, 2024. (Picha na AFP)

Hospitali moja ya Gaza ilisema Jumapili kwamba shambulio la anga la Israel lililolenga nyumba moja katika kambi ya wakimbizi katikati mwa ardhi ya Palestina liliua takriban watu 20.

"Watu 20 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya shambulio la anga la Israel kulenga nyumba ya familia ya Hassan katika kambi ya wakimbizi ya Al-Nuseirat katikati mwa Gaza," Hospitali ya Martyrs ya Al-Aqsa ilisema katika taarifa.

Walioshuhudia walisema shambulio hilo lilitokea mwendo wa saa tisa asubuhi kwa saa za huko. Jeshi la Israel limesema linachunguza ripoti hiyo.

Shirika rasmi la habari la Palestina, Wafa, liliripoti kuwa waliojeruhiwa ni pamoja na watoto kadhaa, na waokoaji walikuwa wakitafuta watu waliopotea na walionaswa chini ya vifusi.

Mapigano makali yameripotiwa katika kambi ya kati ya Nuseirat tangu jeshi lianzishe operesheni inayolenga mji wa kusini wa Rafah mapema mwezi Mei. Wanamgambo wa Kipalestina na wanajeshi wa Israel pia wamepambana katika kambi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza kwa siku kadhaa sasa.

Walioshuhudia walisema nyumba kadhaa zililengwa katika mashambulizi ya anga, wakati wa usiku, kote Gaza, na kwamba mashambulizi ya anga na mizinga, pia yalilenga maeneo ya Rafah wakati wa usiku.

Jeshi la Israel limesema wanajeshi wengine wawili waliuawa huko Gaza siku iliyotangulia. Jeshi lilisema wanajeshi 282 wameuawa hadi sasa katika operesheni ya kijeshi ya Gaza tangu kuanza kwa mashambulizi ya ardhini Oktoba 27.