Waitara ahamia CCM, adai Mbowe - Chadema 'anawatishia'

Freeman Mbowe

Mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, nchini Tanzania, Mwita Waitara amesema amehamia Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe anawatishia wale wanaotaka kugombania nafasi yake ya uwenyekiti licha ya kuwa ameishikilia kwa miaka 20 sasa.

Akitangaza uamuzi wake Jumamosi, Waitara alisema amejiuzulu ubunge na nafasi nyingine zote za uongozi alizokuwa akitumikia Chadema.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutokana na madai ya Waitara, Mbowe alijibu akisema hajawahi kuingia kwenye malumbano wala kugombana na Waitara kama alivyodai lakini kama ameamua kuhama Chadema anamtakia safari njema.

"Hii ni safari ya kisiasa. Kama imani yake imemtuma kuhama Chadema anaruhusiwa kwenda kokote kwa sababu uongozi ni uvumilivu na hakuna chama, taasisi ambayo haina migogoro. Uongozi ni busara na Mungu amsaidie huko anakokwenda,” alisema.

Mbowe alisema wakati Waitara akiondoka CCM alikitukana chama hicho na sasa ameondoka Chadema ameamua kuichafua.

Waitara anakuwa Mbunge wa pili wa Chadema kuhamia CCM na wa tatu kutoka upinzani akitanguliwa na Godwin Mollel (Siha) na Maulid Mtulia (Kinondoni) ambaye awali alikuwa Mbunge wa Chama cha Wananchi (CUF).

Disemba 2, mwaka jana, Mtulia alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo ya ubunge na kufuatiwa na Dkt Mollel Desemba 24.

Katika mkutano wake na vyombo vya habari ofisi ndogo ya CCM mjini Dar es Salaam, Waitara alisema ndani ya Chadema hawaruhusiwi kuhoji chochote na hilo ndilo jambo kubwa.

“Ugomvi wangu na Mbowe ni kwa sababu kuna uchaguzi wa chama. Nilisema tu kwamba huyu mtu ameongoza chama miaka 20 ni umri wa mtu mzima na chama kinaitwa chama cha demokrasia na maendeleo, lakini demokrasia siioni. Baada ya kuhoji kwenye vikao ndani ya chama, imekuwa nongwa,” alisema.

Waitara alitaja jambo jingine ni kuhusu matumizi ya fedha za ruzuku kwamba Chadema inapata Sh. milioni 236 kila mwezi lakini cha kushangaza chama hakina ofisi ya makao makuu, kanda, mkoa wala jimbo.

Kuhusu madai ya kununuliwa, Waitara alisema: “Sijanunuliwa, mimi si mjinga nina shahada. Nimekuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), nilikuwa Katibu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Kinondoni, Katibu CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Mkutano Mkuu.”