Wahamiaji wafa maji wakati wakielekea Ulaya

Boti ya doria ikiwa jirani na mashua waliyopanda wahamiaji wakati wa oparesheni ya uokoaji huko Malta Februari 23, 2024. Picha na Kitini / Vikosi vya Wanajeshi vya Malta / AFP

Gavana wa mkoa wa Saint Louis nchini Senegal amesema watu 24 waliokuwa wakisafiri kwenda Ulaya wamekufa maji kaskazini mwa taifa hilo wakati boti yao iliyokuwa imejaa watu kuzama, shirika la habari la AFP limesema siku ya Alhamisi.

Gavana Alioune Badara Samb amesema miili 24 imepatikana tangu Jumatano baada ya mashua hiyo kupata matatizo katika sehemu hatari kwenye pwani ya kaskazini.

Mlango wa bahari wa Saint Louis, ambao unakutana na Mto Senegal katika bahari ya Atlantiki, ni sehemu hatari yenye mawimbi makubwa na eneo lenye matope mengi sana.

Samb hakusema watu wangapi wamepotea kutoka katika boti hiyo, ambapo walioshuhudia wamesema ilikuwa imebeba zaidi ya watu 300.

Idadi ya watu kadhaa walionusurika wamefanikiwa kufika ufukweni na kujiingiza miongoni mwa wenyeji, na kufanya iwe vigumu kusema ni watu wangapi haswa walihusika, amesema.

Manusura mmoja amesema boti ilikuwa inatokea Camamance na ilikuwa na zaidi ya watu 300 wakati manusura mwingine alisema anakadiria boti ilikuwa na zaidi ya abiria 200.