Papa Francis alaani sauti za wale wanaojitafutia umaarufu kwa kuchochea hofu

Pope Francis akishiriki katika chakula cha mchana kusherehekea Siku ya Maskini Duniani huko Vatican.

Papa Francis alikula chakula cha mchana na mamia ya wakimbizi, maskini na watu wasio na makazi siku ya Jumapili huku akitoa wito wa kuwepo azma mpya ya kuwasaidia wanyonge katika jamii na kulaani  “sauti za wenye kujitafutia umaarufu” zilizopelekea kilio cha watu hao kutaka wasaidiwe.

Francis alisherehekea Siku ya Dunia ya Kanisa Katoliki la Maskini kwa kuwakaribisha takriban maskini 1,300 kwenda Vatican kwa ajili ya Misa maalum na chakula cha mchana. Watoto walimuwekea mikono yao shingoni wakati akiwa ameketi katika moja ya darzeni ya meza zilizokuwepo katka ukumbi wa wageni wa Vatican.

Wakati wa Misa iliyotangulia chakula cha mchana, Francis alilaani utofauti unaoonyeshwa kwa wahamiaji na maskini, na vile vile “wajumbe wa uovu” ambao wanachochea hofu na nadharia za uongo juu ya wahamiaji kwa maslahi binafsi.

“Tusikubali kughilibiwa na kauli za wenye kujitafutia umaarufu, inayotumika kukandamiza mahitaji ya kweli ya watu kwa kutoa masuluhisho rahisi na ya haraka,” Francis alisema.

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika wakati Italia kwa mara nyingine ikiwa katikati ya mjadala wa Ulaya juu ya wahamiaji, huku serikali ya mrengo wa kulia zaidi ya Waziri Mkuu Giorgia Meloni ikishindana na Ufaransa juu ya hatma ya watu waliookolewa katika Bahari ya Mediterranean. Italia ilizuia boti nne za uokoaji kutoingia bandarini kwa siku kadhaa hadi pale iliporidhia kuruhusu boti tatu kuwateremsha wahamiaji wiki iliyopita na kuilazimisha Ufaransa kuiruhusu boti ya nne kuingia nchini mwao.

Ushindani huo uliibua mzozo wa kidiplomasia ambao ulipelekea Ufaransa kusitisha ushiriki wake katika programu ya Ulaya ya mgawanyo wa wahamiaji na kuongeza udhibiti wa mpaka wake na Italia.

Francis alielezea masikitiko yake kwamba vita vya Ukraine vinaongeza dhiki kwa watu maskini, ambao bado wanahangaika kutokana na janga la virusi vya corona, na pia kutokana na majanga ya asili na mabadiliko ya hali ya hewa.