Wahamiaji 89 waliokuwa wanaelekea Ulaya walifariki baada ya boti yao kuzama mapema wiki hii kwenye pwani ya Mauritania, shirika la habari la serikali na afisa wa eneo hilo walisema Alhamisi, huku wengine kadhaa wakipotea.
“Walinzi wa pwani wa Mauritania walipata miili ya watu 89 waliokuwa ndani ya boti kubwa ya mbao ya wavuvi ambayo ilipinduka Julai 1 kwenye pwani ya bahari ya Atlantiki takriban kilomita 4 kutoka mji wa kusini-magharibi mwa nchi wa Ndiago, shirika hilo la habari limesema.
Walinzi wa pwani waliwaokoa watu tisa, akiwemo mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitano, shirika hilo la habari limeongeza.
Shirika hilo la habari limewanuku manusura wakisema kwamba boti hiyo ilisafiri kutoka mpaka wa Senegal na Gambia ikiwa na abiria 170, na idadi ya waliotoweka imefikia 72.
Afisa mkuu wa serikali ya mtaa ametoa taarifa hiyo hiyo kwa shirika la habari la AFP, kwa masharti ya kutotajwa jina.