Waandishi wa habari wa shirika la habari la AFP waliona tukio hilo, huku mivutano ya kisiasa ikiongezeka kabla ya uchaguzi wa rais mwezi ujao.
Wagombea 11 kati ya 13 wa kiti cha rais katika kinyang'anyiro hicho walikuwa wametoa wito kwa wafuasi kuandamana katikati ya eneo la Mei 13 kupinga kile walichokielezea kama "mapinduzi ya kitaasisi" yanayo mpendelea rais aliyeko madarakani Andry Rajoelina.
Lakini maafisa wa polisi waliiingia kuutawanya umati wa mamia kadhaa ya watu kabla haujafika eneo lililopangwa.
Rais wa zamani na kiongozi mkuu wa upinzani Marc Ravalomanana, ambaye alikuwa miongoni mwa waandamanaji, aliondolewa na kupelekwa eneo salama na walinzi wake.
Mkutano huo haukuidhinishwa na mamlaka, na mamia ya vikosi vya usalama vilikuwa vikifanya doria katikati ya mji nyakati za asubuhi.
Wapiga kura nchini Madagascar, moja ya nchi maskini sana duniani licha ya kuwa na maliasili nyingi, watapiga kura kumchagua rais tarehe 9 Novemba.
Rajoelina mwenye umri wa miaka 49, alijiuzulu mwezi uliopita kwa mujibu wa katiba ili kuwania tena urais.
Rais wa Baraza la Seneti alipaswa kuchukua wadhifa huo lakini alikataa kwa "sababu binafsi", na kuacha jukumu hilo kwa "serikali ya pamoja" inayoongozwa na Waziri Mkuu Christian Ntsay, ambaye ni mshirika wa Rajoelina.
Hatua hiyo ilikubaliwa na mahakama ya juu ya nchi hiyo, na kuibua hasira za upinzani.
Rajoelina alichukua madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2009, baada ya mapinduzi yaliyomuondoa Ravalomanana madarakani.
Baada ya kutoshiriki uchaguzi wa mwaka 2013 kutokana na shinikizo la kimataifa, alipigiwa kura kurejea madarakani mwaka 2018.
Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la Reuters.