Waganda waendelea kudadisi umri wa Museveni

Rais Yoweri Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameadhimisha siku yake ya kuzaliwa, Jumamosi 15 2018, japo hana uhakika kuhusu siku na mwaka alipozaliwa.

Wachambuzi wa siasa wanasema kwamba suala la umri wa Rais Museveni limezuwa gumzo kutokana na marekebisho ya katiba yaliyofanyika mwaka 2018, iliyo kuwa inamzuia kugombea urais anapotimiza umri wa miaka 75.

Baada ya minong'ono ya muda mrefu, Museveni alijitangazia kwamba alizaliwa Septemba 15, japo hakuna sherehe zilizofanyika Leo kuadhimisha siku hiyo ya kuzaliwa kwake.

" Ratiba ya rais ya Leo (Jumamosi) ina shughuli nyingi ya mikutano na baadaye hotuba kwa nchi masaa ya jioni" amesema msemaji wa ikulu ya rais ya Uganda Don Wanyama.

Mjadala juu ya umri wa Rais Museveni limekuwepo nchini Uganda kwa mda mrefu, baada ya Museveni kusema kwamba hajui siku, mwezi na mwaka alipozaliwa.

Mwaka 2017, alitangaza kwamba alizaliwa septemba 15, 1944, kwa kile alichodai kwamba akafuata matukio ya kisayansi na historia wakati huo.

Katika kitabu chake cha 'sowing the mastered seed' cha mwaka 2016, Museveni aliandika kwamba watu watatu akiwemo mamake, Esteeri Kokundeka, walimsaidia kujua siku na mwaka alipozaliwa.

Museveni aliandika kwamba mama yake alimwambia kwamba alizaliwa miezi mitatu kabla ya chanjo ya ng'ombe wengi na wakati masikio ya ng'ombe hao yalikuwa yanawekwa alama maalum za utambuzi, na kwamba mlinzi wa siku nyingi aliyeshiriki zoezi la kutoa chanjo kwa ng'ombe hao, alimsaidia kudhinitisha kwamba alizaliwa mwaka 1944.

Hata hivyo, zimekuwepo taarifa kwamba museveni alizaliwa katika hospitali kuu us serikali ya mbarara, lakini anadai kwamba hakuna maandishi ya aina yoyote kumhusu katika hospitali hiyo.

Katika miaka yake yote, Museveni amekuwa ikuiadimisha siku yake ya kuzaliwa kisiri, katika hatua wakosoaji wake wanasema ni ya kuhepa kejeli kutoka kwa raia wa Uganda kuhusu kiongozi wa nchi asiyejua siku kamili aliyozaliwa.

Wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakipinga tarehe anayodai kuzaliwa museveni, wakisema kwamba ni njama tu ya kujipungizia miaka. Wanasiasa wa upinzani wanadai kwamba Museveni alizaliwa Desemba 4, 1937.

Baba yake Rais Museveni, Amos Kaguta, aliaga dunia, Februari 22, 2013 akiwa na umri wa miaka 96, bila kusema lolote kuhusu siku ya kuzaliwa kwa mtoto wake.

Caleb Akandwanaho, ndugu ya Museveni, anayejulilana kama Jenerali Salim Saleh, ana umri wa miaka 58, naye Dr. Violet Kajubiri, dada wa Museveni, anadaiwa kuwa na umri wa miaka 56.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, VOA, Washington DC