Wafanyakazi 6 wa UN wauawa Sudan Kusini

Wananchi wa Sudan Kusini wanakabiliwa na vita na ukame.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa (UN) wamesema kuwa wafanyakazi wanao shughulikia misaada ya kibinadamu walishambuliwa na kuuawa Sudan Kusini.

Maafisa hao wamesema kuwa wafanyakazi hao waliuawa Jumamosi wakati wanasafiri katika msafara kutoka mji mkuu wa Juba wakielekea mji wa mashariki ya Pibor.

“Nimeshtushwa na kukasirishwa kwa mauji haya ya kinyama…,” Eugene Owusu, afisa wa ngazi ya juu wa misaada ya kibinadamu wa UN huko Sudan Kusini amesema.

“Wakati mahitaji ya misaada ya kibinadamu yameongezeka kwa kiwango kikubwa, hili halikubaliki kabisa kwamba wale ambao wanajaribu kutoa msaada wanashambuliwa na kuuawa.”

UN wamesema kuwa mauaji haya yanawakilisha idadi kubwa ya wafanyakazi wanao shughulikia misaada ya kibinadamu waliouawa katika tukio moja, tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipoanza Disemba 2013.

Wafanyakazi wengine 12 waliuawa mwaka huu Sudan Kusini na wengine 79 waliuawa tangu vita hivi vilipoanza.

Shirika la wakimbizi la UN linaripoti kuwa wananchi wa Sudan Kusini milioni 1.6 wamekimbilia nchi jirani kutokana na njaa, vita na ukame, wakiifanya Sudan Kusini kuwa na tatizo la wakimbizi linalo ongezeka kwa kasi duniani.

Shirika la wakimbizi la UN limesema kiwango cha watu walio sambaratishwa kutoka Sudan Kusini inatisha, ikisababisha mzigo mkubwa wa wakimbizi kwa eneo hilo.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe Sudan Kusini imewaondosha zaidi ya watu milioni 3.5 kutoka katika makazi yao ambao wametawanyika ndani na nje ya nchi.

UN inaripoti kuwa watu milioni 4.8 ndani ya nchi wanakabiliwa na njaa, na wengine 100,000 hawana chakula cha kutosha.