Kundi la waasi wa M23 limesonga mbele kwenye uwanja mwingine wa mapambano huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kwa kuteka wilaya mbili katika jimbo la Kivu Kusini, vyanzo vya eneo hilo vimeiambia AFP Jumatano.
Kundi hilo limesonga mbali zaidi baada ya kuchukua udhibiti wa mji muhimu wa Goma huko Kivu Kaskazini kufuatia mapigano makali na wanajeshi wa Congo.
Jumatano asubuhi, waasi wa M23 hawakupata usumbufu wowote kwa kuteka wilaya za Kiniezire na Mukwidja katika jimbo jirani la Kivu Kusini, chanzo cha maeneo hayo na wakazi wamesema.
“Hapakuwa mapigano” wakati wakisonga mbele, amesema kiongozi wa mashirika ya kiraia ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu za kiusalama.
Wakazi kadhaa wa vijiji hivyo viwili waliowasiliana na AFP wamethibitisha kutekwa kwa eneo hilo.