Vyama vya wafanyakazi nchini Guinea vyasitisha mgomo

Kiongozi wa kijeshi wa Guinea, Jenerali Mamady Doumbouya

Vyama vya wafanyakazi nchini Guinea Jumatano vilisema kwamba vimesitisha mgomo wa kitaifa ambao ulidumaza shughuli kwa siku tatu baada ya mwanaharakati mashuhuri wa vyombo vya habari kuachiliwa huru.

Sekou Jamal Pendessa, katibu mkuu wa chama cha wanahabari wa Guinea, alikamatwa mwezi uliopita kwa kuitisha maandamano dhidi ya udhibiti wa vyombo vya habari.

Kuachiliwa kwake Jumatano ilikuwa moja ya madai muhimu ya waandamanaji katika nchi ambako maandamano ni nadra chini ya utawala wa kijeshi wa Jenerali Mamady Doumbouya.

Vyama vya wafanyakazi vilisema katika taarifa kwamba vina nia ya kuanzisha tena mazungumzo kuanzia leo Alhamisi.

Msemaji wa vyama hivyo Abdoulaye Sow, awali alisema kuachiliwa kwa Pendessa inaamisha “ tunaweza kurejea kwenye meza ya mazungumzo na serikali kujadili madai mengine.”

Kupunguza bei ya chakula, kuondoa udhibiti wa vyombo vya habari na kuboresha hali ya maisha ya wafanyakazi wa serikali ni madai waandamanaji wanaomba yashughulikiwe katika mazungumzo yajayo.